MAKALA: Wingu jeusi lagubika mechi kati ya Thika United na Ushuru

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  13:41

Kwa Muhtasari

MAJUMA mawili baada ya kipute cha Ligi Kuu ya KPL kutamatika rasmi, wingu jeusi bado linazingira mchakato wa kuandaliwa kwa mechi za mchujo kati ya Thika United na Ushuru FC kwa nia ya kubaini timu ya tatu itakayoshuka daraja kutoka KPL na nyingine ya tatu itakayokwezwa kushiriki kivumbi hicho mwakani.

 

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kikosi cha Thika United ambacho chini ya kocha Nicholas Muyoti kilikamilisha kampeni za KPL katika nafasi ya 16 kilipangiwa kushiriki michuano miwili ya mchujo dhidi ya Ushuru ambao waliambulia nafasi ya tatu kwenye jedwali la NSL katika jitihada za kusalia ligini kuwania ubingwa wa KPL mwaka ujao.

Hata hivyo, huenda mechi hizo zilizopangwa kusakatwa mnamo Desemba 2 na 6, 2017 zikakosa kupigwa baada ya Muyoti kusisitiza kwamba Thika United walivunja kambi yao na kuwaruhusu wachezaji kuanza likizo pindi baada ya kumenyana na Bandari katika mchuano wa mwisho wa KPL msimu huu.

“Wachezaji wetu walianza likizo yapata majuma mawili yaliyopita baada ya kuvaana na Bandari. Yasikitisha kwamba kufikia sasa sijapokea mawasiliano yoyote rasmi kutoka kwa wahusika kuniarifu kuhusu mipango ya kuwashirikisha Thika United katika michuano miwili ya mchujo dhidi ya Ushuru,” akatanguliza Muyoti kwa kusisitiza kuwa Thika wanapanga kurejea kambini chini ya majuma machache yajayo kwa nia ya kuanza maandalizi ya kunogesha kipute cha KPL mwakani.

“Siwezi kusema lolote kuhusu suala la kushiriki michuano ya mikondo miwili ya mchujo dhidi ya Ushuru. Hilo ni jukumu la usimamizi wa Thika United ambao ni waajiri wangu,” akasema Muyoti ambaye ni nyota wa zamani wa Harambee Stars.

Kwa upande wao, Ushuru ya kocha Ken Kenyatta ilizidi kunoa kucha katika juhudi za kujiandaa kuvaana na Thika United baada ya kuwalazimishia AFC Leopards sare ya 3-3 katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha mnamo Novemba 29, 2017  uwanjani Camp Toyoyo. 
Leopards walitumia mechi hiyo ya jana kama fursa ya kuwafanyia majaribio baadhi ya wachezaji wanaowahemea muhula huu wa uhamisho. 

Wawili kati ya masogora waliofanyiwa jana majaribio na Leopards ni wazawa wa Nigeria.  

Mabao ya Leopards yalifumwa kimiani kupitia kwa mchezaji wa zamani wa Western Stima, Robert Achema, Marselas Ingotsi, Ezekiel Odera.

Ushuru walitikisa nyavu za wapinzani wao kupitia kwa Nelson Marosowe, Benson Amianda na kiungo wa zamani wa Leopards, Mohammed Hassan.

Mapema mwaka wa 2017, FKF ilisisitiza kwamba kikosi kitakachoshikilia nafasi ya 16 katika jedwali la KPL na kingine kitakachomaliza kampeni za NSL katika nafasi ya tatu vitashiriki michuano miwili ya mchujo ili kujipa uhakika wa kuwania ubingwa wa KPL katika msimu ujao.

Ingawa hivyo, suala hilo lilipingwa vikali na KPL ambao kwa mujibu wao wanahisi kwamba FKF inastahili kuheshimu Mkataba wa Maelewano wa 2015 ambapo klabu mbili kutoka KPL zinashushwa ngazi na mbili nyinginezo za NSL kupandishwa daraja mwishoni mwa kila msimu.

Hadi kufikia sasa, Vihiga United na Wazito FC wana uhakika wa kushiriki kivumbi cha KPL mwakani baada ya kutawala jedwali la NSL msimu huu. Western Stima na Muhoroni Youth waliteremshwa ngazi mwishoni mwa msimu huu baada ya kukokota nanga mkiani mwa jedwali la KPL kwa alama 38 na 25 mtawalia.