http://www.swahilihub.com/image/view/-/4924186/medRes/1968277/-/j7ddow/-/mwinyi.jpg

 

Yanga, Zahera ndani ya penzi la kusisimua

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera 

Na Edo Kumwembe

Imepakiwa - Monday, January 7  2019 at  09:42

Kwa Muhtasari

Ameishika Yanga mkononi na anajua kama ameishika Yanga mkononi

 

NI kama umeshika rimoti yako sebuleni. Unatazama filamu ya kusisimua. Imejaa kila aina ya vimbwanga. Ndivyo ninavyomtazama Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera na Yanga yake. Wananipa burudani kabla hata hawajagusa uwanja wa soka.

Zahera ni kocha Yanga, hapo hapo ni Mwenyekiti wa Yanga. Hapo hapo ni Msemaji wa Yanga. Kwa sasa ameishika Yanga mkononi na anajua kama ameishika Yanga mkononi. Watu wa Yanga wanamkubali. Ni kocha gani angewavumilia zaidi ya Zahera? Hakuna kabisa aisee.

Zahera anavumilia matatizo ya Yanga. Siri ya mtungi aijuaye kata. Kuna matatizo ambavyo anayasema hadharani, kuna matatizo ambayo hayasemi. Kocha, ambaye anafuata misingi ya uweledi (Professionalism) katika kazi yake hawezi kuwa Yanga kwa sasa.

Hata hivyo, Zahera bado yupo Yanga na wala haonyeshi dalili ya kuondoka. Ameyavaa matatizo na anayakabili, anayafurahia na anatabasamu nayo. Anacheka nayo, analia nayo kama alivyofanya pale Mbeya.

Kwa mfano, kocha mzungu mwenye weledi wake angekuwa ameshaikimbia klabu ambayo hailipi mishahara kwa wakati kwa wachezaji wake. Angekuwa ameshaikimbia klabu ambayo wachezaji wake hawana uhakika wa kusafiri kwenda kucheza mechi zake za Ligi Kuu.

Lakini, Zahera ndio kwanza anajirekodi akiwa Ufaransa akiomba mashabiki waichangie klabu ili nauli ya ndege ipatikane timu isafiri kwenda Mbeya. Na kweli, mashabiki wanaichangia timu, inasafiri, inafika, inashinda mechi yake.

Hapo Zahera ameifanya kazi ya uenyekiti, usemaji. Kocha wa Kizungu angeikimbia klabu hii lakini Zahera yupo tu. Ndio kwanza anawahamasisha wachezaji wake wacheze na washinde mechi. Wale ambao wanakuwa wavivu anawafokea. Anapata wapi ujasiri wa kuwazodoa wachezaji wavivu wasiolipwa mishahara? Hapo ndio ujue kuna Zahera mmoja tu duniani.

Nasikia kuna mshambuliaji ambaye, Yanga walikuwa wanamtaka kutoka Kenya. Zahera mwenyewe akatoa ahadi ya kutoa Dola 10,000 kama mchango wake ili mshambuliaji huyo atue Yanga. Umeona wapi kocha akiongeza pesa ya usajili ili kununua mchezaji?

Siku nyingine nasikia anawapa wachezaji pesa zake za mfukoni kama wakimfurahisha. Nasikia alifanya hivyo Mbeya. Huyu ndiye Zahera ambaye ananifurahisha. Kisa? Anafurahi jinsi alivyoikamata klabu kubwa kama Yanga mkononi. Wakongo wanapenda sifa na anajua jinsi anavyoendelea kukaa Yanga ndivyo anavyojipatia umaarufu.

Zahera ni kocha wa shida Yanga. Kitu ambacho nina uhakika nacho, Yanga ikipata pesa itaachana na Zahera. Hizi timu pacha za Kariakoo hazijawahi kuwa na fadhila kwa wachezaji wao, viongozi wao wala makocha wao. Ngoja Yanga ipate pesa ndipo utajua tabia zao halisi.

Kama yule tajiri wa Yanga akirudi ndipo watu wa Yanga watakapoanza kudai Zahera anaropoka ovyo kwa wachezaji. Watakwambia timu haichezi poa hata kama inashinda. Na ni kweli, sio kwamba Yanga inacheza mpira wa kusisimua sana, lakini inashinda mechi zake.

Vitaibuka visingizio vingi tu kama Yanga ikipata pesa. Ghafla ataletwa kocha mzungu kutoka Serbia kimya kimya. Zahera hataamini anachokiona. Haya yote ambayo yanatokea kwa sasa atahisi ni kama ndoto tu. Wakubwa wa Kariakoo sio watu wa kuwaamini hata kidogo.

Lakini, kwa sasa acha Zahera atambe. Kwa hali iliyopo klabuni kwa sasa Zahera ndiye kocha mwafaka zaidi Jangwani. Nani ataivumilia Yanga ya leo zaidi ya Zahera? Zahera anajua hili ndio maana watoto wa uswahilini tunasema ‘Anajimwayamwaya’. Amewakamata mkononi. Kwa sasa yeye ndiye Yanga na Yanga ndio yeye. Huwa inatokea mara chache katika maisha ya mwanadamu kuikamata mkononi klabu kama Yanga au Simba.

Jaribu kutazama alichofanya kwa kipa wa Yanga, Beno Kakolanya. Zamani mabosi wa Yanga wasingempa Zahera kauli ya mwisho kuhusu Beno. Wangeweza kumwamuru lazima Beno arudi kikosini, lakini Zahera kasimama kidete.

Amemvua unahodha Kevin Yondani na kumpatia Ibrahim Ajibu. Zamani maamuzi haya lazima yachukuliwe na uongozi na sio Zahera peke yake. kwa sasa mabosi wa timu hawawezi kwenda tofauti sana na Zahera kwa sababu wana hofu ya kumpoteza. Watampata wapi kocha kama Zahera? Kocha ambaye atawavumilia na kusogeza siku mbele. Kocha, ambaye anawaomba mashabiki waichangie timu tiketi za ndege na kweli inawezekana. Wao wenyewe hawawezi kusikilizwa na mashabiki katika kiwango ambacho Zahera anasikilizwa kwa sasa.

Na ndio maana nafurahia kushika rimoti yangu na kuitazama filamu ambayo inaendelea Jangwani. Zahera akizungumza kitu lazima nimsikilize. Kuna wakati anaongea kama kocha wa Yanga, kuna wakati anaongea kama msemaji wa Yanga, kuna wakati anaongea kama shabiki wa Yanga. Raha iliyoje jamani.

Sijui kitu gani kitakuja kumuondoa Yanga, lakini siku moja Yanga itatazama nyuma na kumuenzi sana mtu anayeita Mwinyi Zahera. Hatakumbukwa kwa aina ya soka wanalilocheza katika enzi zake. Atakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa kila kitu Yanga. Mwenyewe kwa sasa anaifurahia hali hii. Acha aifurahie tu. Mwanadamu anaishi mara moja tu.