http://www.swahilihub.com/image/view/-/5068454/medRes/2310881/-/77cogxz/-/yanga+pic.jpg

 

Yanga haiachi kitu

Na Saddam Sadick na Masoud Masasi, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, April 12  2019 at  12:03

 

Mwanza. Kitendo cha beki nguli Kelvin Yondani kupewa kadi nyekundu ni miongoni mwa matukio yaliyojiri katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya Yanga na Kagera Sugar.

Yanga jana ilishinda mabao 3-2 dhidi ya Kagera Sugar huku mshambuliaji nyota Heritie Makambo akiendelea kufunga mabao katika mashindano hayo.

Mechi hiyo ilikuwa ya pili kwa Yanga kupata pointi tatu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baada ya kuilaza African Lyon mabao 2-0 katika mechi ya awali.

Makambo aliongeza kasi ya kuwania kiatu cha ufungaji bora, baada ya kufunga bao lake la 15 na kumpiku nyota wa Simba Meddie Kagere mwenye mabao 14. Salim Aiyee wa Mwadui Shinyanga anaongoza kwa mabao 16.

Matokeo hayo yameongeza pengo la pointi katika msimamo wa ligi ambapo imefikisha pointi 74 ikifuatiwa na Azam yenye pointi 63 na Simba 57.

Yanga ilifanya kazi ya ziada kupata pointi tatu katika mchezo huo kutokana na ubora wa Kagera Sugar ambayo jana ilicheza kwa nguvu dakika zote 90. Shujaa wa Yanga katika mchezo huo alikuwa kiungo Mzimbabwe Thabani Kamusoko aliyefunga bao la ushindi kwa kiki kali ya mpira wa faulo. Mabao mengine yalifungwa na Makambo na Kassim Hamisi aliyejifunga.

Yanga ilipata pigo dakika ya 81 baada ya beki wake nguli Kelvin Yondani kupewa kadi nyekundu na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro kwa kumchezea madhambi Hamisi.

Mechi ilivyokuwa.

Yanga ilifanya shambulizi dakika ya 22 baada ya Makambo kupiga kiki kali iliyodakwa na kipa wa Kagera Sugar Jeremia Kisubi.

Paul Ngalyoma aliipatia Kagera Sugar bao la kwanza kwa kichwa dakika ya 30 akimalizia mpira wa kona uliopigwa na Ally Ramadhani. Yanga ilipata bao la kwanza dakika ya 33 baada ya kona iliyopigwa na Kamusoko kutua kichwani kwa Tshishimbi na mpira kumchanganya Hamisi aliyejifunga katika harakati za kuokoa. Dakika ya 47 Makambo alifunga bao la pili kwa mpira wa kichwa akimaliza pasi iliyopigwa mbali na Yondani. Hamisi alisahihisha makosa baada ya kufunga bao la pili dakika ya 57 kwa kiki kali iliyompita kipa Klausi Kindoki. Yanga iliendelea kupambana na kupata bao la tatu lililofungwa na Kamusoko dakika ya 74 kwa mpira wa adhabu iliyokwenda wavuni. Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera alisema mechi ilikuwa ngumu kwa kuwa bado wachezaji wake wana uchovu wa kucheza mechi mfululizo.

Yanga: Klausi Kindoki,Paul Godfrey, Gadiel Michael, Andrew Vincent,Kelvin Yondani, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Papy Tshishimbi, Heritier Makambo, Thabani Kamusoko na Jaffari Mohammed.

Kagera: Jeremia Kisubi,Mwaita Gereza, David Luhende, Juma Nyosso, Juma Shemvuni, Peter Mwalyanzi, Kassim Hamis, Ally Ramadhani, Omary Mponda, Paul Ngalyoma na Venace Ludovick.