http://www.swahilihub.com/image/view/-/4339656/medRes/1907427/-/k3umc9z/-/yanga.jpg

 

Yanga yaishika pabaya Simba

Yanga

Shabiki wa klabu ya Yanga timu hiyo ilipocheza dhidi ya Bunamwaya ya Uganda kuwania Kagame Castle Cup Julai 2, 2011, uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Tanzania/MAKTABA 

Na CHARLES ABEL, Mwananchi cabel@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  12:08

Kwa Muhtasari

Yanga imetafuna vyema mfupa uliowashinda Simba na kuwaweka watani wao wa jadi kwenye presha kubwa, katika mbio za kuwania ubingwa baada ya kuibuka na ushindi muhimu dhidi ya Stand United.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

YANGA imetafuna vyema mfupa uliowashinda Simba na kuwaweka watani wao wa jadi kwenye presha kubwa, katika mbio za kuwania ubingwa baada ya kuibuka na ushindi muhimu dhidi ya Stand United.

Mashabiki wa Yanga walitoka Jumatatu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam roho kwatu baada ya kushuhudia timu yao ikipata ushindi wa mabao 3-1.

Stand United iliivimbia Simba kwa kulazimisha sare ya mabao 3-3, katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja huo wiki iliyopita.

Yanga imekaa patamu katika msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kufikisha pointi 46 sawa na Simba, lakini iko nafasi ya pili baada ya kuzidiwa kwa uwiano wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Timu hiyo imepunguza pengo la pointi nane lililokuwepo awali huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi na Simba itakuwa faida ya michezo miwili.

Ushindi wa Yanga umeongeza presha kwa Simba ambayo haina rekodi nzuri ya kutanua pengo la pointi dhidi ya Yanga inapokuwa imetangulia mbele kwa pointi chache.

Msimu uliopita Simba ilishindwa kudhibiti pengo la pointi tano dhidi ya Yanga licha ya kubaki michezo sita ya ligi lakini ilikosa ubingwa.

Simba ilipoteza pointi tano kati ya michezo sita ikifungwa na Kagera Sugar, ilitoka sare na Toto Africans na kulingana pointi na Yanga mwishoni mwa msimu. Simba ilikosa ubingwa kwa tofauti ya uwiano wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Mchezo huo ulikuwa wa mwisho kwa Yanga kabla ya kwenda Botswana kuvaana na Township Rollers katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Machi 17, baada ya Yanga kuchapwa mabao 2-1 katika mchezo wa awali. Yanga ilitarajiwa kusafiri usiku wa kuamkia leo kwenda mjini Gaborone, Botswana.

Katika mchezo wa Jumatatu, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, walitumia muda wa dakika tano kipindi cha kwanza kufunga mabao mawili ya haraka yaliyowavuruga wachezaji wa Stand United.

Licha ya kuanza mchezo huku kikosi chake kikiwa na mabadiliko kadhaa. Yanga ilikuwa na kiu ya kupata ushindi huo muhimu ambao unawaweka katika nafasi nzuri ya kuwatibulia Simba kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Rafael Daud, Maka Edward, Juma Abdul na Gadiel Michael walianza katika mchezo kuchukua nafasi za Haji Mwinyi, Emmanuel Martin, Hassani Kessy, Pato Ngonyani na Thabani Kamusoko walioanza kwenye mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar.

Mchezo ulivyokuwa

Yanga ilitakata tangu dakika ya mwanzo ya mchezo na kuipa kazi ya ziada Stand United kucheza kwa tahadhari muda wote wa mchezo.

Ubora huo wa Yanga ulizaa matunda baada ya kupata bao la mapema dakika ya saba lililofungwa na kinda Yusuph Mhilu kwa njia ya krosi ambayo iliokolewa vibaya na beki wa Stand United, Erick Mulilo  kabla ya mpira kujaa wavuni.

Stand United ambayo ilianza mchezo na mabeki watano, ilishindwa kuhimili mashambulizi ya Yanga na dakika tano baadaye ilijikuta ikiruhusu bao la pili lililofungwa na Ibrahim Ajibu aliyemalizia kwa ustadi pasi ya Daud.

Yanga ilitumia vyema udhaifu wa Stand United kujaza idadi kubwa ya wachezaji kwenye safu ya ulinzi, kutawala mpira na kutengeneza nafasi za mabao ambazo kama zingetumiwa vyema ingepata ushindi mnono.

Stand United ilianza kucheza madhambi ya mara kwa mara na kusababisha kumaliza dakika 45 kipindi cha kwanza ikiwa na kadi mbili za njano zilizotolewa kwa wachezaji Blaise Bigirimana na Aron Lulambo kupitia kwa mwamuzi Clemence Manga kutoka Njombe.