http://www.swahilihub.com/image/view/-/5144190/medRes/2362908/-/uckq9d/-/yanga+pic.jpg

 

Yanga yanasa kifaa Namibia

Na Majuto Omary, momary@tz.nationmedia.com

Imepakiwa - Tuesday, June 4  2019 at  10:28

 

Dar es Salaam.  Mshambuliaji nyota wa timu ya taifa ya Namibia inayojiandaa ya michuano ya Afcon, Sadney Urikhob yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na klabu ya Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Wakati Urikhob ajiandaa kumwaga wino kuichezea klabu hiyo, nyota wa zamani wa klabu hiyo, Gadiel Michael amesaini mkataba wa miaka mitatu kwa kuendelea kukipiga kwa wakali hao wa mitaa ya Jangwani na Twiga.

Habari zilizoifikia Mwananchi jana, zilisema kuwa Urikhob alitarajiwa kuwasili nchini jana usiku na kusaini mkataba wa miaka miwili na kurejea katika kambi ya timu yake ya Taifa inayojiandaa na michuano ya Afcon.

Taraifa zimesema kuwa Urikhob alikwisha malizana na mmoja wa viongozi wa Yanga wakati akiwa Namibia na kinachofanyika sasa ni kukamilisha dili la usajili huo pia.

Sambamba na Urikhob ambaye aliwahi kuchezea timu ya Amazulu ya Afrika Kusini pamoja na klabu za Saraburi,  Super Power Samut Prakan,  BEC Tero Sasana (zote za Thailand) na PSMS Medan  ya Indonesia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu ya Yanga, Frank Kamugisha alisema kuwa kimsingi wamekwisha maliza mazungumzo na mchezaji huyo na ujio wake ni kumalizia makubaliano.

Alisema kuwa sambamba na Urikhob ni beki wa timu ya Taifa ya Burundi,  Mustapha Suleiman ambaye alitarajiwa kuondoka nchini jana.

“Sadney kwa sasa (jana) yupo njiani anakuja nchini, tunamtarajia kuingia hapa saa moja usiku (jana), ni mchezaji mwenye uzoefu na tulimfuatilia, Alifanya vyema sana katika mashindano ya Cosafa na michuano mingine akiwa na timu ya Taifa,” alisema Kamugisha.

Alisema kuwa wanafanya usajili wao kwa umakini mkubwa na wanatarajia kuwa na kikosi kipana kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Tumeweka mipango mkakati, tunataka kumaliza usajili kabla ya zoezi kumalizika ili tuanze maandalizi mengine. Tumejipanga kufanya mambo makubwa msimu ujao. Tunaomba wanachama, mashabiki na wadau wa timu kutuunga mkono,” alisema.

Mpaka sasa, Yanga imekwisha sajili wachezaji saba wa kigeni. Wachezaji hao ni Lamine Moro ambaye ni raia wa Ghana,  Issa Bigirimana, Patrick Sibomana (Rwanda), Kalengo Maybin (Zambia) na  Mustapha Seleman kutoka Burundi.

Katika orodha hiyo wamo akina Papy Kabamba Tshishimbi aliyeongeza mkataba wake na Klaus Kindoki ambao bado ana mkataba na timu hiyo. Pia kuna mchezaji mzawa,  Abdul Aziz Makame kutoka Zanzibar.