http://www.swahilihub.com/image/view/-/4122230/medRes/1769170/-/acsl51/-/hg.jpg

 

Young Dragon wa Thika wapiga hatua kubwa katika Karate

Young Dragon

Vijana wa karate wa klabu ya Young Dragon. Picha/LAWRENCE ONGARO 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Tuesday, October 3  2017 at  09:05

Kwa Muhtasari

Klabu ya Karate ya Young Dragon Karate Academy imejizadidi kuona ya kwamba inazidi kutamba katika mchezo huo mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.

 

KLABU ya Karate ya Young Dragon Karate Academy imejizadidi kuona ya kwamba inazidi kutamba katika mchezo huo mjini Thika, Kaunti ya Kiambu.

Kocha wake Elizabeth Rukwaro anasema ya kwamba klabu hiyo ilibuniwa miaka minne iliyopita.

Kwa sasa anajivunia kuwa na vijana chipukizi wapatao 43.

"Chipukizi hao wana umri wa kati ya miaka minne hadi 17 na wote wamedumisha nidhamu ya hali ya juu," alisema Rukwaro.

Alisema lengo lake kuu la kuhakikisha vijana wana nidhamu na kujituma katika maisha bila kushurutishwa na yeyote.

Alisema jambo la kutia moyo ni kwamba aliwatoa vijana hao kutoka makazi ya mabanda kama Kiandutu, Kiganjo, Landless na Athena mjini Thika.

"Lengo langu kuu lilikuwa ni kuwaondoa katika maovu na kuwaingiza katika maadili mema maishani," asema Rukwaro.

Anazidi kueleza ya kwamba kazi hiyo ya kuwanoa chipukizi hao ni ya kujitolea bila kulipwa hata senti moja na wazazi wao.

"Matumaini yangu ni kuona ya kwamba ninakuza kizazi kilicho na nidhamu na maadili mema na hiyo ndiyo furaha yangu," alisema Rukwaro.

Alisema mazoezi yake huendeshwa kati ya Jumatatu hadi Ijumaa huku wakipumzika Jumamosi na Jumapili.

Alizidi kueleza ya kwamba kinachompa kichocheo cha kuwa na chipukizi hao ni kwa sababu ya "wazazi wao kunipa mwelekeo mwema wa kuwanoa watoto hao".

"Hata wazazi wengi kuchukua jukumu la kufika katika ukumbi wa shule ya msingi ya Kenyatta ili kuwatazama wana wao wakirusha mateke ya karate," asema Rukwaro.

Mashindano Afrika

Mwaka wa 2014 kocha Rukwaro alisafiri na wanakarate wanane hadi Afika Kusini kwa mashindano ya karate ya Afrika.

Kocha Rukwaro anaiomba kaunti ya Kiambu chini ya gavana mpya Ferdinand Waititu kuingilia kati na kufanya juhudi ya timu hiyo kupiga hatua zaidi.

"Mwezi huu wa Oktoba 2017, ninajiandaa kusafiri na wanakarate watatu katika mashindano ya dunia ya Funakoshi yatakayofanyika London, Uingereza kwa wiki moja mfululizo," alisema Rukwaro.

Wanakarate hao wanaojiandaa kusafiri katika mashindano hayo ni Elizabeth Njeri, Rehema Achieng' na James Marori.

Anasema bado wanatafuta wahisani kujitokeza ili kununua tikiti za ndege kwa chipukizi hawa.