Zanzibar U-17 yafukuzwa kutoka kwa mashindano nchini Burundi

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Monday, April 16  2018 at  16:37

Kwa Muhtasari

Timu ya taifa ya Zanzibar imefukuzwa kutoka mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Burundi na kupigwa faini ya Sh1,509,825 za Kenya (Sh 34,024,500 za Tanzania).

 

TIMU ya taifa ya Zanzibar imefukuzwa kutoka mashindano ya soka ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 nchini Burundi na kupigwa fainai ya Sh1,509,825 za Kenya (Sh 34,024,500 za Tanzania).

Hii ni baada ya kupatikana na kosa la kuwasilisha majina ya wachezaji tisa waliozidi umri huo kwa mechi ya Sudan.

Baada ya kufanya ufichuzi huo, Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limetangaza Jumatatu kwamba limepiga Zanzibar marufuku kushiriki mashindano yote inayoandaa hadi pale itakapolipa faini ya Sh1,509,825 za Kenya (Sh 34,024,500 za Tanzania).

Fedha hizi, kulingana na Cecafa, zitarejeshwa katika Shirikisho la Soka duniani (FIFA) ambalo ni wadhamini wakuu wa makala ya mwaka 2018.

Taarifa kutoka Cecafa zimesema kwamba timu ya Zanzibar inafaa kuchukua ndege ya kwanza itakayopatikana ya kurudi Tanzania. Kuondolewa kwa Zanzibar katika makala haya ya tatu kunabakiza timu saba mashindanoni. Zanzibar ilikuwa kundi B pamoja na Uganda (mabingwa watetezi), Tanzania na Sudan. Mechi kati ya Zanzibar na Sudan haikuchezwa kutokana na udanganyifu huo. Uganda na Tanzania zilitoka 1-1. Kenya, Somalia, Ethiopia na wenyeji Burundi wako katika Kundi A. Mabingwa wa makala ya kwanza Burundi walibwagwa 4-0 na Kenya katika siku ya kwanza ya mashindano Aprili 14. Ethiopia, ambayo ilishinda Somalia 3-1, iliishia kupoteza mchuano huo kwa mabao 3-0 dhidi ya Somalia baada ya kupatikana imechezesha wachezaji watatu waliopitisha umri wa miaka 17. Mbali na kupokonywa ushindi, Ethiopia pia imepigwa faini ya Sh502, 970 za Kenya.