http://www.swahilihub.com/image/view/-/4758160/medRes/2109021/-/oh9gvl/-/zalika.jpg

 

Zarika aweka bayana nia yake kustaafu masumbwi

Fatuma Zarika

Mkenya Fatuma Zarika (kati) asherehekea baada ya kumshinda Yamileth Mercado wa Mexico Septemba 8, 2018, Nairobi wakati wa kabiliano la WBC uzani wa Super-bantam kwa wanawake. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, September 13  2018 at  18:31

Kwa Muhtasari

Fatuma Zarika ambaye ni bingwa mpya wa dunia wa masumbwi ya wanawake katika uzani wa kilo 55.3 (Super Bantam), ametangaza atastaafu miaka miwili ijayo.

 

NAIROBI, Kenya

BINGWA mpya wa dunia wa masumbwi ya wanawake katika uzani wa kilo 55.3 (Super Bantam), Fatuma Zarika ametangaza Alhamisi atastaafu miaka miwili ijayo.

Bondia huyu Mkenya mwenye umri wa miaka 34 almaarufu Iron Fist, alitolewa kijasho chembamba na chipukizi matata Yemileth Mercado, 20, kabla ya kushinda raia huyo wa Mexico kwa wingi wa pointi 96-94, 97-93 na 99-91 jijini Nairobi hapo Septemba 8 katika pigano la raundi 10.

“Bingwa wa taji la masumbwi ya wanawake ya dunia ya WBC wa uzani wa Super Bantam Fatuma Zarika, ambaye alihifadhi taji lake kwa mara ya pili kwa kumlima Yemileth Mercado hapo Septemba 8 jijini Nairobi, ametangaza atastaafu mwaka 2020 na anapanga kuwa kocha,” mtandao wa kijamii wa Wizara ya Michezo ya Kenya, umeripoti.

Zarika, ambaye alishinda taji hili la WBC kwa mara ya kwanza mwaka 2016, ni mmoja wa mabingwa wanne katika uzani huu.

Wengine ni Yazmin Rivas kutoka Mexico (WBA), raia wa Argentina Marcela Eliana Acuna (IBF) na Dina Thorslund kutoka Denmark (WBO).