http://www.swahilihub.com/image/view/-/4883940/medRes/1903018/-/x5oajf/-/nick.jpg

 

Ndio tumefuzu kushiriki Afcon, lakini tunataka barua rasmi - FKF yaambia CAF

Nick Mwendwa

iRais wa Shirikisho la Kandanda nchini Kenya, Nick Mwendwa, akihutubia wanahabari awali katika makao makuu ya chombo hicho. Picha/CHRIS OMOLLO 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, December 6  2018 at  13:32

Kwa Muhtasari

Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa amefichua kwamba chombo hicho kingali kinasubiri kupokea barua rasmi kutoka kwa Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) ndiposa iamini timu ya wanaume ya Harambee Stars itashiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2019.

 

NAIROBI, Kenya

UAMINIFU kati ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) na Shirikisho la Soka la Bara Afrika bado ni tete baada ya Kenya kutangaza Alhamisi kwamba inahitaji barua rasmi kutoka kwa CAF ndiposa iamini timu ya wanaume ya Harambee Stars itashiriki Kombe la Afrika (Afcon) mwaka 2019.

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Rais wa FKF Nick Mwendwa amesema kwamba Kenya haitaki kushuhudia masaibu yaliyoipata timu ya wanawake ya Harambee Starlets.

“Tumeitisha kikao hiki na wanahabari kuwaeleza kuhusu mashindano ya AFCON 2019. Kenya imefuzu kushiriki Afcon kwa sababu Sierra Leone imepigwa marufuku. Sierra Leone ilikuwa imepigwa marufuku na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), marufuku ambayo CAF ilithibitisha kwa baada ya kamati yake kuu kukutana jijini Accra nchini Ghana (Novemba 30, 2018). Marufuku dhidi ya Sierra Leone ilimaanisha kwamba matokeo yote ambayo Kenya, Ghana na Ethiopia kwenye Kundi F yalifutiliwa mbali. Kundi hili limesalia na timu tatu – Kenya, Ghana na Ethiopia, ambazo zimezoa alama saba, sita na moja mtawalia baada ya Sierra Leone kuondolewa.

“Tumewasiliana na CAF tukiitaka ituandikie rasmi barua kuhusu kufuzu kwetu. Hatutaki kilichotutendeka katika Kombe la Afrika la wanawake (AWCON) kitufike tena. Kisheria, Kenya tumeshafuzu kushiriki AFCON mwaka 2019, lakini tunataka ithibati ya barua ya kuonyesha hivyo ili mambo yasigeuke kuwa kama Harambee Starlets ambayo tuliruhusiwa kushiriki Awcon halafu siku chache kabla ya mashindano yenyewe tukaondolewa,” Mwendwa amesema jijini Nairobi.

Kushtaki Guinea ya Ikweta

Kenya ilishtaki Equatorial Guinea kwa kuchezesha mchezaji ambaye si halali katika mechi za kufuzu kushiriki Awcon nchini Ghana mwaka 2018 zilizosakatwa mwezi Juni. Ilishinda kesi dhidi ya Equatorial Guinea na kupewa tiketi badala ya Equatorial Guinea. Hata hivyo, baada ya kutaja kikosi na hata kuzamia maandalizi, CAF ilitangaza kurejeshwa kwa Equatorial Guinea kwenye Awcon na kuondolewa kwa Kenya. Tukio hilo lilifanya Kenya kukimbia katika mahakama ya michezo (CAS) kutaka mashindano hayo yaliyofanyika Novemba 17 hadi Desemba 1 yasimamishwe hadi iruhusiwe kushiriki. Ilipoteza kesi hiyo na mashindano hayo ya mataifa manane yaliendelea jinsi ilivyopangwa. Hata hivyo, Kenya imesema itaendelea kutafuta haki kwa sababu haikupewa nafasi ya kujieleza wala kufahamishwa kwamba Equatorial Guinea ilikuwa imekata rufaa dhidi ya kutimuliwa kutoka AWCON. “Bado tunatafuta haki sio tu kuhusu maswala ya kurejeshewa fedha tulizotumia kuweka kikosi kambini, bali ni kutafuta haki. Kenya tulinyimwa haki yetu,” amesema Mwendwa.