http://www.swahilihub.com/image/view/-/4296208/medRes/1879552/-/dkinoiz/-/okwi.jpg

 

Hii ndio Simba ya kimataifa

Emmanuel Okwi

Emmanuel Okwi ambaye ni mzawa wa Uganda huchezea klabu ya Simba nchini Tanzania. Picha/MAKTABA 

Na MWANDISHI WETU

Imepakiwa - Tuesday, February 13  2018 at  06:45

Kwa Muhtasari

Timu ya Simba imepeleka makali ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa.

 

TIMU ya Simba imepeleka makali ya Ligi Kuu Tanzania Bara katika mashindano ya kimataifa.

Simba imecheza kwa kiwango bora katika mashindano ya Ligi Kuu tangu kuanza msimu huu, sasa imepania kushiriki kufanya kweli kimataifa baada ya kushindwa kutamba kwa miaka mitano.

Wachezaji wa timu hiyo wameonyesha nia ya kutaka mafanikio msimu huu baada ya kuiweka Simba kileleni kwa pointi 41, katika msimamo wa Ligi Kuu.

Simba Jumapili ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Gendermarie ya Djibout katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mashabiki wa Simba walitoka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam roho kwatu baada ya Simba kucheza kwa kiwango bora mchezo huo.

Muungano mzuri wa safu ya ushambuliaji wa nahodha John Bocco na Emmanuel Okwi, ulinogeshwa na viungo Said Ndemla na Jonas Mkude waliokuwa na kazi moja ya kupenyeza mipira mbele.

Okwi licha ya kufunga bao katika mchezo huo, alikosa idadi kubwa ya mabao licha ya kupata nafasi nzuri za kufunga.
Hata hivyo, mchezo huo sio kipimo kwa Simba katika mashindano ya kimataifa kwani Gendermarie si timu bora ya ushindani.
Simba ina nafasi kubwa kupepetana na El Masry ya Misri katika mchezo wa raundi ya kwanza baada ya timu hiyo jana kuilaza Green Buffaloes ya Zambia mabao 4-0.
Mchezo wa marudiano baina ya Simba na Gendermarie, unatarajiwa kuchezwa Februari 21.

Mchezo ulivyokuwa

Simba iliingia uwanjani ikionekana na lengo moja tu la kupata ushindi mnono ili uwaweke katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo na hilo lilijidhihirisha na uamuzi wa benchi la ufundi kurudia mfumo wa 3-5-2 huku wakijaza idadi kubwa ya wachezaji ambao kiasili wamekuwa bora katika kushambulia.

Mpango huo wa Simba ulionekana kutimia dakika ya kwanza ya mchezo baada ya kupata bao la kuongoza kupitia kwa Said Ndemla ambaye alipiga mkwaju wa faulo uliokwenda moja kwa moja nyavuni.

Faulo hiyo ilizawadia Simba baada ya Bocco kuangushwa na mmoja wa mabeki wa Gendermarie.

Kuingia bao hilo ni kama kuliathiri mpango wa Simba, baada ya hapo kina Bocco walikosa umakini na ubunifu kila waliposogelea lango la wapinzani wao hatua iliyochangia kupoteza idadi kubwa ya nafasi za mabao ambazo walitengeneza huku kila mmoja akionekana kutaka kufunga.

Iliwachukua takribani dakika 30 washambuliaji wa Simba kukaa sawa hasa baada ya Bocco kuifungia bao ka pili na kuanza kucheza kwa utulivu kabla ya mchezaji huyo kufunga tena dakika ya 45.

Hata hivyo, tabia ya Simba kujisahau kipindi cha pili nusura iwaponze baada ya wapinzani wao kupata penalti iliyotokana na makosa ya Erasto Nyoni aliyecheza faulo ndani ya eneo la hatari, lakini hata hivyo mkwaju uliopigwa na Hussein Migane uliokokewa kwa ustadi na kipa Aishi Manula.

Baada ya Gendermarie kupoteza penalti hiyo, wachezaji wake walioneyesha uhai na kujaribu kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba ambayo ililazimika kufanya mabadiliko ya kuwatoa Shiza Kichuya na Ndemla na kuingia Muzamiru Yassin na Mwinyi Kazimoto ili kuimarisha safu ya kiungo.

Wakati wengi wakiamini mechi hiyo ingemalizika kwa matokeo ya ushindi wa 3-0, Okwi aliwainua vitini mashabiki wa Simba dakika za majeruhi baada ya kumalizia kwa shuti kali la chinichini mpira wa faulo aliotengewa na Kazimoto.
Kocha Simba

“Tunashukuru Mungu hatukuruhusu bao, ushindi ni ushindi kwa sababu mabao manne sio machache,” alisema Kocha Msaidizi wa Simba Masoud Djuma.