http://www.swahilihub.com/image/view/-/3822964/medRes/1570530/-/i7ah6rz/-/lekop.jpg

 

Chan Yuen-ting kuweka historia kuongoza wanaume Klabu Bingwa

Chan Yuen-ting

Kocha mrembo Chan Yuen-ting wa klabu ya wanaume ya Ligi Kuu ya Hong Kong, Eastern, atabasamu baada ya mazoezi Hong Kong, Mei 11, 2016. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Wednesday, February 22  2017 at  10:13

Kwa Muhtasari

Chan Yuen-ting ataweka rekodi nyingine ya dunia katika soka kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza klabu ya soka ya wanaume katika Klabu Bingwa Asia, Jumatano saa tisa alasiri.

 

MREMBO Chan Yuen-ting ataweka rekodi nyingine ya dunia katika soka kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza klabu ya soka ya wanaume katika Klabu Bingwa Asia, Jumatano saa tisa alasiri.

Kulingana na shirika la habari la AFP, Yuen-ting, 28, ataongoza mabingwa wa Ligi Kuu ya Hong Kong, Eastern, dhidi ya mabingwa mara mbili wa Asia, Guangzhou Evergrande kutoka Uchina.

Mwaka 2016, Mchina huyo anayefahamika kwa jina la utani kama Beef Ball alikuwa kocha wa kwanza kabisa mwanamke duniani kushinda Ligi Kuu akinoa timu ya wanaume.

Mafanikio yake yalifanya ashinde tuzo ya Kocha bora wa mwaka 2016 barani Asia na pia kuingia katika orodha ya shirika la BBC ya wanawake 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.

Mabingwa mara sita wa Ligi Kuu ya Uchina, Evergrande, wanaongozwa na kocha mtajika Luiz Felipe Scolari.

Vijana wa Scolari wanasaka kushinda taji la tatu la Asia katika kipindi cha miaka mitano.

Evergrande imepata motisha baada ya bilionea Hui Kayan, ambaye ni mwenyekiti na mmiliki wa klabu hiyo, kuahidi marupurupu ya Sh4.5 bilioni kwa kila ushindi watavuna katika Klabu Bingwa.

Ni mara ya kwanza kabisa Eastern inashiriki Klabu Bingwa.

Yuen-ting alianza kunoa Eastern mwaka 2015 baada ya kufunza timu ya taifa ya Hong Kong kati ya mwaka 2008-2013.