Harambee Starlets U-17 yajiondoa kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Thursday, October 5  2017 at  13:22

Kwa Muhtasari

Kenya imejiondoa katika mechi za mchujo za kushiriki Kombe la Dunia la wanawake wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2018 zilizopangiwa kung’oa nanga Oktoba 13, 2017 na kukamilika Februari 18, 2018.

 

KENYA imejiondoa katika mechi za mchujo za kushiriki Kombe la Dunia la wanawake wasiozidi umri wa miaka 17 mwaka 2018 zilizopangiwa kung’oa nanga Oktoba 13, 2017 na kukamilika Februari 18, 2018.

Taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imesema Alhamisi kuwa shirikisho hilo haliwezi kuunda kikosi kwa sababu wachezaji watakuwa wakifanya mtihani wa mwisho wa mwaka.

“Tumeandikia mashirikisho ya soka ya Dunia (FIFA) na Afrika (CAF) kuyafahamisha hali yetu,” amesema Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Robert Muthomi.

“Mnavyojua, tulikuwa tumepangiwa kuchapana na Ethiopia mnamo Oktoba 13 na Oktoba 27 mwaka 2017. Hata hivyo, baada ya kushauriana na maafisa kutoka Wizara ya Elimu, tumeamua kuondoa ushiriki wetu ili kuwapa wachezaji muda wa kutosha kujiandaa kwa mtihani wao, ambao pia ni muhimu katika kujiendeleza maishani mwao,” alieleza Muthomi.

Awamu ya kuingia raundi ya kwanza inaleta pamoja mataifa 10.

Baada ya Kenya kujiondoa, mataifa yatakayolimana katika awamu hiyo ya kuingia raundi ya kwanza ni Algeria, Botswana, Djibouti, Gambia, Libya, Mali, Sierra Leone na Zambia.

Kujiondoa kwa Kenya kumeipa Ethiopia tiketi ya kusonga katika raundi ya kwanza ambayo ina mataifa ya Cameroon, Equatorial Guinea, Ghana, Morocco, Nigeria, Afrika Kusini na Tunisia.

Ethiopia italimana na Nigeria katika raundi ya kwanza mwezi Desemba.