http://www.swahilihub.com/image/view/-/4930780/medRes/2221273/-/x5ubij/-/oli.jpg

 

Watunisia na Mtanzania kusimamia mechi ya Gor na New Star ya Cameroon

Dennis Oliech

Mshambuliaji Dennis Oliech wa Gor Mahia katika hii picha ya Januari 6, 2019, Gor Mahia ilicheza dhidi ya Mathare United uwanjani Kasarani, Nairobi, Kenya. Picha/CHRIS OMOLLO 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, January 11  2019 at  13:14

Kwa Muhtasari

Mechi ya mkondo wa kwanza ya mwondoano ya Kombe la Mashirikisho la Afrika kati ya Gor Mahia na New Star kutoka Cameroon itasakatwa, Jumapili, Januari 13, 2019, katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

 

NAIROBI, Kenya

MECHI ya mkondo wa kwanza ya mwondoano ya Kombe la Mashirikisho la Afrika kati ya Gor Mahia na New Star kutoka Cameroon itasimamiwa na maafisa kutoka Tunisia - Haythem Guirat (refa), Yamen Malloulchi (mnyanyuaji kibendera wa kwanza), Khalil Hassani (mnyanyuaji kibendera wa pili) na Walid Djeridi (afisa wa nne).

Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) limetaja Mtanzania Ahmed Iddi Mgoyi kuwa kamishna wa mechi hii itakayosakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Januari 13.

“Maafisa hawa wametua nchini Ijumaa, Januari 11 asubuhi tayari kwa mechi itakayosakatwa Jumapili kuanzia saa kumi jioni,” taarifa kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) imesema.

Kwa mujibu wa FKF, New Star kutoka mjini Doula itawasili Ijumaa saa nne usiku na kupata fursa ya kufanyia mazoezi uwanjani Kasarani hapo Jumamosi jioni kabla ya kuvaana na mabingwa mara 17 wa Kenya, Gor mnamo Jumapili.

Ada

Mashabiki watalipia Sh200 kutazama mechi kutoka sehemu za kawaida za uwanja huku watu mashuhuri wakinunua tiketi zao kwa Sh500. Tiketi za mechi zitapatikana katika maeneo ya Kenya Cinema, kituo cha polisi cha Ngomongo, mkabala wa hoteli ya Safari Park pamoja na milango nambari 12 na 2 katika uwanja wa Kasarani.

Mshindi kati ya Gor na New Star baada ya mechi ya marudiano kusakatwa Januari 20 ataingia mechi za makundi za mashindano haya ya klabu ya pili kwa ukubwa baada ya Klabu Bingwa Afrika.