Matangazo ya kubeti marufuku

Na CLEDO MICHAEL, Mwananchi

Imepakiwa - Monday, January 28  2019 at  12:40

Kwa Muhtasari

Michezo ya kubahatisha imedaiwa kupotosha vijana wengi wa mataifa ya Afrika Mashariki.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

BODI ya Michezo ya Kubahatisha (GBT) imezuia kwa muda urushaji wa matangazo ya michezo ya kubahatisha kupitia redio na televisheni kwa maelezo kuwa yamekithiri kiasi cha kuharibu taswira ya mchezo huo.

Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya viongozi wa dini kulalamika kuwa michezo hiyo inaharibu vijana na kusababisha wasifanye kazi. Pia imekuja wakati Rais Yoweri Museveni wa Uganda amepiga marufuku michezo hiyo inayosambaa kwa kasi duniani.

Taarifa ya Januari 23 iliyosainiwa na kaimu mkurugenzi mkuu wa bodi hiyo, James Mbalwe imeeleza kuwa hatua hiyo inatokana na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu kukithiri kwa matangazo kwenye vyombo hivyo vya habari.

“Kumekuwa na ongezeko la malalamiko kutoka kwa umma juu ya kukithiri kwa matangazo ya michezo ya kubahatisha hapa nchini,” inasema taarifa hiyo.

“Bodi imesitisha kwa muda urushaji wa matangazo ya michezo ya kubahatisha kupitia redio na televisheni. Matangazo yanayotolewa kupitia vyombo vingine hayaathiriwi na zuio hili.”

Januari 23 ni siku ambayo Rais John Magufuli alikutana na viongozi wa dini, na mmoja wao, Zainuddin Adamjee kutoka Jumuiya ya Mabohora, alilalamikia suala la michezo ya kubahatisha.

Kiongozi huyo alisema anashangazwa na tabia ya vyombo vya habari kufanya matangazo ya michezo ya kubahatisha licha ya kuwa ni haramu katika dini zote.

Adamjee alisema hivi sasa vijana wengi nchini ambao ni nguvu kazi ya Taifa wanacheza kamari kila dakika kwa sababu kila ukifungua televisheni ni matangazo ya michezo hiyo.

“Mambo mengi yanazungumzwa hivi sasa ni kamari tu. Kauli yako ya ‘hapa kazi tu’ kwa hizi kampuni ni ‘hapa kamari tu’. Utaona vijana wengi badala ya kufanya kazi wanacheza kamari,” alisema.

Taarifa ya GBT inasema kwa mujibu wa maagizo ya Rais yaliyotolewa mara baada ya kikao hicho, imeamua kusitisha matangazo ya michezo hiyo hasa kwenye redio na televisheni.

GBT imesema ina mpango wa kuitisha mkutano na wadau Jumatano ijayo ili kujadili namna bora ya uendeshaji wa michezo hiyo hususan kwenye matangazo.

“Lazima tutambue kukithiri kwa matangazo kuna hatarisha uhamasishaji unaozingatia uwajibikaji na hivyo kunaharibu taswira ya michezo ya kubahatisha,” inasema taarifa hiyo.

 

Kampuni zasubiri kikao

Viongozi wa kampuni zinazoendesha michezo hiyo hawakuwa tayari kuzungumzia suala hilo zaidi ya kusubiri kikao.

“Nasubiri kikao chetu na bodi ili kujadili suala hili,” alisema mkurugenzi mtendaji wa Biko, Charles Mgeta ambaye hata hivyo alisema wataendelea na biashara hiyo.

“Tunatarajia kwenda kuzungumzia hiyo issue (suala) tarehe 30 Januari na hapo tutaangalia kipi kina tija au hakina tija. Uamuzi utakavyokuwa ndivyo tutakavyoendelea na biashara.”

Mmoja wa wadau waliohojiwa na Mwananchi, alisema kubeti si tatizo ni ajira.

“Kama wanaona kubeti ni kubaya, tutafutiwe ajira,” alisema.