http://www.swahilihub.com/image/view/-/2869540/medRes/1118614/-/jo33r8/-/696004-01-02.jpg

 

Ratiba ya 2016 mbio za Diamond League yatolewa

Eunice Jepkoech Sum

Eunice Jepkoech Sum wa Kenya asherehekea baada ya kushinda mkondo wa Zurich mbio za mita 800 na kutwaa taji la Diamond League Septemba 3, 2015. Picha/AFP 

Na GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

Imepakiwa - Saturday, December 19  2015 at  13:19

Kwa Muhtasari

Ratiba ya mashindano ya riadha ya Diamond League ya msimu 2016 imetangazwa ambapo Wakenya Asbel Kiprop, Jairus Birech, Eunice Sum na Virginia Nyambura watasaka kuhifadhi mataji yao.

 

RATIBA ya mashindano ya riadha ya Diamond League ya msimu 2016 imetangazwa ambapo Wakenya Asbel Kiprop, Jairus Birech, Eunice Sum na Virginia Nyambura watasaka kuhifadhi mataji yao.

Bingwa mara tatu wa dunia Kiprop atatetea taji la mita 1500, bingwa wa Afrika Birech (mita 3000 kuruka viunzi na maji), bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola Sum (mita 800) na bingwa wa Michezo ya Olimpiki ya Chipukizi mwaka 2010 Nyambura (mita 3000 kuruka viunzi na maji).

Nyambura alianzia safari yake ya kutwaa taji la ligi hii jijini Doha mnamo Mei 15 akitimka kwa saa 9:21.51 na atasaka kulitetea.

Sum atasaka taji lake la nne mfululizo katika ligi hiyo baada ya kushinda mwaka 2013, 2014 na 2015. Birech naye anajivunia mataji ya mwaka 2014 na 2015. 

Mashindano haya yanayojumuisha duru 14 yataanzia jijini Doha nchini Qatar mnamo Mei 6 na kukamilika jijini Brussels nchini Ubelgiji mnamo Septemba 9.

Washindi wa vitengo 32 vitakavyowaniwa watatia kibindoni tuzo ya Sh4 milioni na kombe rembo kila mmoja.

Baada ya kutawala Riadha za Dunia jijini Beijing nchini Uchina mwezi Agosti, macho yatakuwa kwa Wakenya mnamo 2016 ambapo wanariadha wengi watatumia Ligi ya Almasi kujinoa kabla ya Michezo ya Olimpiki jijini Rio de Janeiro nchini Brazil mnamo Agosti 5 hadi Agosti 21.

 

Ratiba ya mwaka 2016:

Doha, Qatar (Mei 6), Shanghai, Uchina (Mei 14), Eugene, Marekani (Mei 28), Rome, Italia (Juni 2), Birmingham, Uingereza (Juni 5), Oslo, Norway (Juni 9), Stockholm, Sweden (Juni 16), New York, Amerika (Juni 18), Monaco, Ufaransa (Julai 15), London, Uingereza (Julai 22-23), Lausanne, Uswizi (Agosti 25), Paris, Ufaransa (Agosti 27), Zurich, Uswizi (Septemba 1) na Brussels, Ubelgiji (Septemba 9).