http://www.swahilihub.com/image/view/-/4298406/medRes/1880960/-/hi2wl9/-/fanzi.jpg

 

Sekunde tatu zamponza Fancy Chemutai

Fancy Chemutai

Mwanariadha Fancy Chemutai. Picha/MAKTABA 

Na GEOFFREY ANENE

Imepakiwa - Friday, February 9  2018 at  16:47

Kwa Mukhtasari

Fancy Chemutai alikosa tuzo ya kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya Sh10 milioni kwa sekunde tatu baada ya kushinda Ras Khaimah Half Marathon kwa saa 1:04:53 katika Milki za Kiarabu, Ijumaa.

 

FANCY Chemutai alikosa tuzo ya kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 ya Sh10 milioni kwa sekunde tatu baada ya kushinda Ras Khaimah Half Marathon kwa saa 1:04:53 katika Milki za Kiarabu, Ijumaa.

Rekodi ya dunia ya saa 1:04:51 inashikiliwa na Joyciline Jepkosgei tangu mwaka 2017.

Hata hivyo, Chemutai alijizolea Sh1, 379,728 kwa kumaliza katika nafasi ya kwanza na kuongezwa Sh496, 702 kwa kuvunja rekodi ya Ras Khaimah Half Marathon ya saa 1:05:06 iliyoshikiliwa na mshindi wa mwaka 2017, Mkenya mwenzake Peres Jepchirchir.

Chemutai aliongoza Wakenya kufagia nafasi tano za kwanza. Alimaliza sekunde mbili mbele ya bingwa wa mwaka 2011, 2012 na 2015, Mary Keitany, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42.

Caroline Kipkurui (1:05:07), Joan Chelimo Melly (1:05:37) na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21, Jepkosgei (1:06:46) walifuatana kutoka nafasi ya tatu hadi tano, mtawalia. Nambari mbili hadi tano walizawadiwa Sh962, 427, Sh687, 448, Sh494, 962 na Sh412, 468, mtawalia. Degitu Azimeraw (Ethiopia, 1:06:47), Brigid Kosgei (Kenya, 1:06:49), Gladys Cherono (Kenya, 1:07:13), Helen Bekele (Ethiopia, 1:07:47) na Naom Jebet (Kenya, 1:08:22) walitunukiwa Sh274,979, Sh206,234, Sh151,238, Sh96,242 na Sh54,995, mtawalia. Walimaliza katika nafasi za sita, saba, nane, tisa na 10, mtawalia.

Kenya ilichukua nafasi 13 kati ya 15 za kwanza kwenye kitengo cha wanaume ambacho bingwa mtetezi Bedan Karoki alihifadhi taji lake. Mkenya huyu alitumia dakika 58:42 akifuta rekodi ya Ras Khaimah Half Marathon ya 58:52 iliyowekwa na Mkenya Patrick Makau mwaka 2009.

Muethiopia Jemal Yimer (59:00) na Wakenya Alex Kibet (59:06), Jorum Lumbasi (59:36), Morris Gachaga (59:36), Wilfred Kimitei (59:40), Edwin Kiptoo (59:54), Bernard Kimeli (saa 1:00:16) na Vincent Rono (1:00:24) na raia wa Ethiopia Lelisa Desisa (1:00:28) walinyakua nafasi tisa zilizofuata, mtawalia.