http://www.swahilihub.com/image/view/-/3522822/medRes/1538619/-/d7g9f9z/-/nyua.jpg

 

Kuna matumaini kwa timu tano za Afrika katika Kombe la Dunia?

Essam El-Hadary

Golikipa wa Misri, Essam El-Hadary kwenye mazoezi Port-Gentil Januari 18, 2017. Picha/AFP 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  10:54

Kwa Muhtasari

  • Udadisi wa kina ni kuwa, ni timu tatu za bara Afrika ambazo zimeshawahi kutinga robo fainali ya dimba hilo katika historia yake
  • Timu hizo ni Cameroon mwaka wa 1990 nchini Italia, Senegal ikajipa hadhi hiyo ya robo mwaka wa 2002 nchini Korea Kusini na Japan, na hatimaye Ghana mwaka wa 2010 nchini Afrika Kusini

 

WAWAKILISHI wa Afrika katika kinyang'anyiro cha kuwinda taji la Kombe la Dunia katika soka kinachong’oa nanga kesho Alhamisi ni Misri, Morocco, Tunisia, Nigeria, na Senegal.

Udadisi wa kina ni kuwa, ni timu tatu za bara Afrika ambazo zimeshawahi kutinga robo fainali ya dimba hilo katika historia yake.

Timu hizo ni Cameroon mwaka wa 1990 nchini Italia, Senegal ikajipa hadhi hiyo ya robo mwaka wa 2002 nchini Korea Kusini na Japan na hatimaye Ghana mwaka wa 2010 nchini Afrika Kusini.

Kuna dukuduku kuwa marefarii huwa na ubaguzi kwa timu za Afrika na ambapo mara kwa mara uamuzi wanaotoa ugani huonekana wa kuchochea timu hizo zing’oke mapema.

Cameroon iking’oka katika robo fainali 2002 ilikuwa ni kwa bahati mbaya ambapo ilitikisiwa nyavu zake na Uingereza kukibakia tu dakika saba mchezo uishe na ni refarii aliyetoa penalti iliyojaa utata.

Penalti hiyo ilisawazisha mambo na katika muda wa ziada, mambo yakaishia kuwa 3-2 na Cameroon ikaaga mashindano.

Senegal nayo mwaka wa 2002 iling’olewa kwa ‘goli la dhahabu’ dakika nne tu ndani ya muda wa ziada.

Ghana ndiyo ilisononesha nyoyo nyingi Afrika na mashabiki wake kwingine duniani kwa kuwa ikimenyana na Uruguay 2010, mshambulizi wa Uruguay, Luis Suarez alitumia mkono wake kusimamisha mpira uliokuwa unaelekea nyavuni na ambapo timu hii ya Afrika ingesonga mbele.

Hata hivyo, Asamoah Gyan alipokabidhiwa jukumu la kutwanga mkwaju wa penalti uliotolewa, alipoteza. Uruguay ikasonga mbele, Ghana ikaabiri ndege kurejea kwao.

Jeraha

Wakati huu, Misri inategemea uwezo na umahiri wa Mohamed Salah mbele ya goli na ambapo amedhihirisha uwezo wake mkuu wa kuzititiga nyavu akichezea timu yake ya Liverpool nchini Uingereza.

Ingawa anauguza jeraha, mashabiki wake na wa Misri sawia na wa Liverpool hawataki kuwazia timu hii ya Pharaohs ikiwa haina Salah.

Nyani wao, Essam El-Hadary akiwa na umri wa miaka 45 ana wajibu wa kukupa ushahidi kuwa 'mzee ni wewe' na kocha wao ni Héctor Cúper kutoka Argentina.

Katika kundi la A, Misiri itamaliza udhia katika michuano ya makundi na wenyeji Urusi, Saudi Arabia na Uruguay.

Morocco wako kwa fomu ya kipekee ambapo walifuzu kwa dimba hilo bila kupoteza mechi hata moja au kufungwa goli hata moja.

Ikiwa na kocha Hervé Renard ambaye ni Mfaransa, hatari ni kuwa katika kundi lao la B, kuna Uhispania, Ureno, na Iran. Hapa, wadadisi wanasema kuwa wanaomba tu uwasamehe kwa kuwa kuna uwezekano wa 'msiba' mapema wa Morocco kuaga mapema.

Nigeria ilikuwa timu bora zaidi barani Afrika na iliyokuwa na wafuasi wengi ikifahamika hadi sasa kama Super Eagles. Wako katika kundi lingine hatari ambapo lina Argentina, Iceland na Croatia katika kundi la D.

Tunisia nao katika kundi la G watamenyana na Ubelgiji, Uingereza, na Panama.

Hapa kuna matumaini kulingana na wadadisi kwa kuwa timu hizi zote hakuna inayoonekana ikiwa bora zaidi au mbaya zaidi kuliko nyingine, upatu ukipewa Uingereza kuongoza kundi na Tunisia hapa inaweza ikajipa nafasi ya pili ya kusonga mbele, au hata iongoze kundi hilo. Kocha wao, Nabil Maâloul ameelezea matumaini yake ya kufanya vyema.

Senegal ina ile taswira ya kupendeka na mashabiki. Iko na vipaji kama Sadio Mane wa Liverpool na mwenzake wa Napoli, Kalidou Koulibaly bila kusahau Keita Baldé wa Monaco. Kuna Yule Idrissa Gana Gueye wa Everton na wakiwa na kocha Aliou Cissé, Uafrika kamili unajiangazia na ni timu ya kutazamwa kwa makini ikimenyana na wapinzani katika kundi H ambapo kuna wa uwezekano mkuu wa kupepeteka wakiwa ni Japan, Poland, na Colombia.