http://www.swahilihub.com/image/view/-/4564722/medRes/412869/-/jjlbff/-/Wenger.jpg

 

Vumbi la Wenger lazoa sita Arsenal

Arsene Wenger

Kocha Arsene Wenger. Picha/AFP 

Na MASHIRIKA

Imepakiwa - Wednesday, May 16  2018 at  13:52

Kwa Muhtasari

Zikiwa ni siku chache baada ya Arsenal kumpa mkono wa kwaheri kocha Arsene Wenger, kambi ya Emirates imeendelea kufanya mabadiliko makubwa kwenye benchi lake la ufundi.

 

LONDON, Uingereza

SIKU chache baada ya Arsenal kumpa mkono wa kwaheri kocha Arsene Wenger, kambi ya Emirates imeendelea kufanya mabadiliko makubwa kwenye benchi lake la ufundi.

Viongozi wa klabu hiyo wamewaondoa maofisa sita waliokuwa wasaidizi wa kocha huyo aliyedumu kwa miaka 22 klabuni hapo.

Panga la maofisa hao limeonekana linalenga kumpa fursa kocha ajaye ndani ya klabu hiyo kuunda safu yake mpya, ambayo atafanya nayo kazi siku za usoni.

Muhanga wa kwanza baada ya Wenger kuondoka ni Boro Primorac, ambaye alikuwa ni kocha wa kikosi cha kwanza cha Arsenal.

Primorac alijiunga na Arsenal, mwaka mmoja baada ya ujio wa kocha huyo Mfaransa ndani ya timu hiyo, akitokea klabu ya Nagoya Grampus Eight ya Japan alikokuwa kifanya kazi pamoja na Wenger.

Klabu hiyo pia imetangaza kuachana na Mkuu wa Idara ya Matibabu, Colin Lewin ambaye amedumu kwa muda mrefu zaidi ya Wenger ndani ya Arsenal akiwa amefanya kazi kwenye kitengo cha tiba kwa miaka 23.

Mbali na Primorac na Lewin, wengine walioonyeshwa mlango wa kutokea ndani ya Arsenal ni kocha mwingine wa kikosi cha kwanza, Neil Banfield, Mkufunzi wa Makipa, Gerry Peyton, Kocha wa Viungo, Tony Colbert pamoja na mtunza vifaa, Paul Johnson.

Hata hivyo panga hilo linaonekana kuwapitia mbali, Kocha Msaidizi wa Arsenal, Steve Bould na Kocha wa Makipa, Jens Lehmann.

Kwa sasa Arsenal inahaha kusaka kocha mpya atakayerithi mikoba ya Wenger, ambapo majina matatu yameonekana kupewa nafasi ambayo ni manahodha wao wa zamani Patrick Vieira na Mikel Arteta pamoja na kocha wa TSG Hoffenheim, Julian Nagelsmann.