http://www.swahilihub.com/image/view/-/3467416/medRes/1499472/-/114xv8lz/-/ramogi.jpg

 

Raila aanza kujiimarisha kuing'oa Jubilee, akutana na wazee wa jamii tofauti

Ramogi

Kinara wa Cord Raila Odinga alipotawazwa shujaa wa jamii ya Waluo katika Mlima wa Ramogi, Novemba 26, 2016. Picha/TOM OTIENO 

Na BMJ MURIITHI

Imepakiwa - Sunday, January 1  2017 at  14:40

Kwa Mukhtasari

KINARA wa Cord Raila Odinga ameanzisha msururu wa mikutano na wazee kutoka jamii mbalimbali kama njia mojawapo ya kujitafutia uungwaji mkono kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

 

Wiki iliyopita, Bw Odinga alikutana na wazee kutoka jamii za Waluo, Wakalenjin, Abagusii na Wakuria jijini Kisumu ambao baadaye waliahidi kumuunga mkono katika kinyanganyiro cha urais.

Zaidi ya wazee 70 kutoka kaunti 10 za Nyanza na Bonde la Ufa walikuwa wamealikwa na mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Waluo Willis Opiyo Otondi na Katibu Mkuu Owino Nyady.

Wazee hao walitoka katika Kaunti za Kisumu, Siaya, Migori, Homabay, Kisii, Nyamira, Kericho, Bomet, Nandi na Narok.

Akizungumza wakati wa mahojiano na Swahilihub, Katibu wa Baraza Kuu la Wazee wa Jamii ya Kipsigis Edwine Kimetto alisema waliamua kumuunga mkono Bw Odinga kutokana na juhudi zake za kupigania uhifadhi wa Msitu wa Mau.

Bw Kimetto pia alisema juhudi za Bw Odinga kutaka kusimamishwa kwa ujenzi wa mradi wa bwawa la Itare unaogharimu Sh38 bilioni, pia ziliwafanya kuunga mkono kiongozi huyo wa ODM.

Bw Kimetto alisema wazee wa jamii yake watahusika katika kuhimiza wakazi wa maeneo hayo kumpigia kura Bw Odinga 'kwani yeye ndiye atapigania maslahi yetu’.

Kiongozi huyo wa upinzani amekuwa akisisitiza kuwa mradi huo wa Itare huenda ukasababisha uharibifu katika hifadhi ya Masai Mara hivyo kuathiri mapato yanayotokana na sekta ya utalii.

Kulingana na Bw Odinga, mradi huo utafanya mito 12, ukiwemo Mto Mara, kutoka katika Kaunti nane, kukauka hivyo kuhatarisha Msitu wa Mau.

Kumpigia 'Baba' debe

Bw Kimetto alisema wazee hao sasa wataandaa msururu wa mikutano ya kisiasa kumpigia debe Bw Odinga.

“Tayari tumepanga mkutano wa kwanza wa uzinduzi katika eneo la Sosiot, Kaunti ya Kericho Januari 7, mwaka huu, ambapo tumealika Bw Raila Odinga pamoja na viongozi wengineo akiwemo gavana wa Kericho,” akasema Bw Kimetto.

Alisema wazee hao watatumia mkutano huo kueleza jamii ya wanajamii wa Kipsigis kuhusu mwelekeo wanaofaa kuchukua katika kinyang’anyiro cha urais.

Bw Otondi alisema baada ya mkutano huo wa Sosiot wazee hao kwa pamoja watazuru mradi huyo wa Itare Januari16 kabla ya kuelekea mahakamani kuzuia ujenzi wa bwawa hilo.

Mzee Otondi alisema kuwa baraza lake litawafikia wazee kutoka maeneo ya Magharibi kwa lengo la kumpigia debe Bw Odinga.

Bw Odinga ni miongoni mwa viongozi wa upinzani, Kalonzo Musyoka (Wiper), Moses Wetang’ula (Ford-Kenya) na kiongozi wa chama Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi ambao wanamezea mate kiti cha urais kupitia muungano wa kisiasa wa National Super Alliance (NASA).