Kutawazwa kwa Mudavadi kwamkosesha Raila usingizi

Kiongozi wa Cord Raila Odinga

Kiongozi wa Cord Raila Odinga akihutubia wanahabari awali. Picha/EVANS HABIL 

Na ISAAC ONGIRI Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Wednesday, January 4  2017 at  18:45

Kwa Mukhtasari

KIONGOZI wa Cord Raila Odinga, Jumatano alifanya msururu wa mikutano na baadhi ya viongozi kutoka Magharibi mwa nchi katika juhudi za kutuliza joto la kisiasa eneo hilo baada ya kutawazwa kwa kinara wa ANC, Musalia Mudavadi kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

 

Jumatano asubuhi, Bw Odinga alimtembelea kinara mwenzake Seneta Moses Wetangula nyumbani kwake Karen, Nairobi, katika kile kilitajwa kama 'kujipanga kabla ya uchaguzi mkuu 2017.’

Mkutano wao ulijiri saa chache baada ya Bw Mudavadi kukutana na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho mjini Mombasa.

Inasemekana Bw Odinga alimtembelea Bw Wetang’ula ili kumhimiza aendelee kuunga Cord licha ya Bw Mudavadi kurudi katika upinzani.

Uhasama kati ya Wetang’ula na Mudavadi umezua hofu katika upinzani kwamba serikali inaweza kuutumia kugawanya kura za eneo la Magharibi ambazo ni muhimu kwa upinzani kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Baada ya kukutana na Bw Odinga, Bw Wetang’ula alikutana na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na aliyekuwa mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo.

Duru zinasema kuwa Bw Odinga na Wetangula waliwaarifu viongozi wenzao kuhusu mipango ya kuanza msururu wa mikutano ya kisiasa kote nchini kupigia debe upinzani katika uchaguzi mkuu ujao.

Bw Odinga alifika nyumbani kwa Bw Wetang’ula ambapo walipata kiamsha kinywa pamoja.

Ukombozi wa mwisho

Jumatano, mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed alisema, kilele cha mikutano ya viongozi tofauti wa upinzani kitakuwa ni “ukombozi wa mwisho wa Kenya kutoka meno ya ufisadi.”

“Ufisadi utaunganisha Wakenya wanaotaka kuona nchi hii ikikombolewa, na ndio sababu viongozi hawa wanafanya kila wawezalo kuhakikisha Kenya inaelekea upande mmoja,” alisema.

Wiki iliyopita, Wetang’ula na Seneta wa Siaya James Orengo walialikwa kwa kiamsha kinywa nyumbani kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka pia katika mtaa wa Karen.

Kupitia ujumbe wa twitter, chama cha Ford Kenya kilisema kwamba, Bw Wetang’ula na Bw Odinga walijadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na uchaguzi mkuu wa 2017.

Kumekuwa na hofu kwamba Bw Wetang’ula amekuwa akitengwa huku Raila akimkumbatia Mudavadi aliyetawazwa msemaji wa jamii ya Waluhya.

Jumatano, seneta wa Kakamega Boni Khalwale aliandika kwenye Twitter kwamba Bw Wetang’ula alikutana na Bw Raila, kisha akakutana na Bw Musyoka na Bw Jirongo.

Naibu kiongozi wa ANC Ayub Savula aliye mbunge wa Lugari alithibitisha kuwa viongozi wa upinzani wanapanga mikutano ya pamoja kote nchini.