Uhuru na Joho wakabana koo Pwani

Ali Hassan Joho

Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho. Picha/MAKTABA 

Na  G. BOCHA na BRIAN OCHARO

Imepakiwa - Friday, January 6   2017 at  13:40

Kwa Mukhtasari

RAIS Uhuru Kenyatta na Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho Alhamisi walionyeshana ubabe wa kisiasa wakati wa uzinduzi wa daraja eneo la Buxton, Mombasa.

 

Bw Joho ambaye alikuwa wa kwanza kuhutubia wananchi katika eneo la Ziwa la Ng’ombe, alimtaka Rais Kenyatta kuelezea miradi iliyoanzishwa na serikali ya Jubilee badala ya kujivunia miradi ya serikali ya 'nusu mkate’ pamoja na wafadhili.

Alisema huu ukiwa mwaka wa siasa, kila mmoja hana budi kujinadi kwa wapiga kura kuhusu miradi ya maendeleo aliyowafanyia na kutaka utawala wa Rais Kenyatta kuelezea kile ambacho serikali yake imewafanyia wakazi wa Mombasa.

“Nimefurahi kuungana na Rais na ujumbe wake waliotutembelea leo kuzindua mradi huu. Na mimi ninafahamu historia ya mradi huu ulioanzishwa 2010 na miradi mengine chini ya Kenya Municipal Programme,” akaeleza Bw Joho.

“Niko kwenye jukwaa hili kuomba kura yangu na ile ya Cord, na Jubilee iko hapa kutafuta kura yake. Hii ni demokrasia na hakuna uhasama.

Tumefanya haya kwa heshima ndiposa tuko kwenye jukwaa moja licha ya tofauti za maoni,” akasema.

Gavana huyo alisema serikali ya Jubilee inastahili kuwaelezea wenyeji wa Mombasa kile ilichowafanyia badala ya kuzindua miradi iliyoanzishwa na utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga.

Rais amefeli

Alisema utawala wa Rais Kenyatta haujaanzisha miradi yoyote ya maendeleo kaunti ya Mombasa. Lakini Rais Kenyatta alishangaa kama wanaosema serikali yake haijafanya lolote Mombasa na sehemu nyingine za Pwani wana macho.

Alisema utawala wake umeanzisha miradi kadha ya maendeleo kama vile soko jipya Kongowea, ukarabati wa soko la Macknoon, ujenzi wa barabara kadha mjini Mombasa na maeneo mengine ya Pwani.

Rais Kenyatta alisema siasa duni hazitaleta maendeleo nchini.

“Hatuna vita na yeyote na hatutaendelea kujibizana na kuhatarisha maisha ya watu wetu. Ukiwa tayari, njoo tufanye kazi pamoja na kama hutaki, basi wacha kila mmoja wetu afanye kazi yake kivyake,” akaeleza Rais Kenyatta.

Rais alisema miradi ya kivuko cha miguu cha Buxton, bomba la maji taka la Bamburi na upanuzi wa makazi ya Ziwa la Ngo’mbe imegharimu Sh3.2 bilioni kupitia ufadhili wa serikali kuu, serikali za Uswizi, Ufaransa na Benki ya Dunia.

Rais alisema serikali ya Jubilee haijatenga Pwani katika maendeleo na kuahidi kurudi Mombasa kufungua soko la nyama na lile la Macknoon, maarufu kama Marikiti.

Waziri wa Utalii Najib Balala Naibu wa gavana wa Mombasa Hazel Katana, wabunge Gideon Munga’ro (Kilifi Kusini), Gonzi Rai (Kinango), Masoud Mwahima (Likoni) walihudhuria hafla hiyo.