http://www.swahilihub.com/image/view/-/4657494/medRes/2040823/-/hiop6w/-/jaji.png

 

NEC yahaidi kujisafisha na kuwaondoa hofu wapinzani

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage (kushoto) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa tume hiyo, Athuman Kihamia (katikati) na mjumbe wa NEC, Jaji Thomas Mihayo wakati wa mkutano na wadau wa vyama vya siasa uliofanyika jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis  

Na Waandishi Wetu

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  12:56

Kwa Muhtasari

Changamoto zinatokana na kutozingatia taratibu, kanuni na sheria

 

Dar/Tanga: Wakati Kamati Kuu ya CCM ikimpitisha Christopher Chiza kugombea ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itahakikisha inaondoa kasoro zilizojitokeza katika chaguzi za marudio zilizopita.

Uchaguzi mdogo unaohusisha ubunge Jimbo la Buyungu wilayani Kakonko unatarajiwa kufanyika sambamba na ule wa kata 79, Agosti 12.

Jimbo la Buyungu liko wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Kasuku Bilago (Chadema) aliyefariki dunia Mei 26. Pia uchaguzi huo utahusisha udiwani kwenye kata hizo zilizopo katika Halmashauri 43 kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara.

Akizungumza wakati akitangaza uchaguzi huo unaotarajiwa kugharimu kiasi cha Sh3 bilioni, mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema jana kuwa changamoto kubwa ni utambulisho wa mawakala.

Changamoto hiyo ni miongoni mwa zilizolalamikiwa na wapinzani katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha pamoja na kata nane, uliofanyika Februari 17.

Malalamiko mengine ya kambi hiyo yalihusu mawakala wao kuzuiwa kuingia katika vyumba vya kupigia kura, chama tawala kuwatumia viongozi wa Serikali katika kampeni, viongozi hao kutumia magari ya umma katika mikutano ya kampeni, vitisho na wagombea wa upinzani kunyimwa fursa ya kushuhudia upigaji kura vituoni.

Hata hivyo, Jaji Kaijage alisema jana kuwa wajibu wa utambulisho wa mawakala katika vituo vya kupigia kura siyo wa vyama vya siasa, bali ni wa msimamizi wa uchaguzi katika jimbo husika au wasaidizi wao.

“Hatutarajii vyama vya siasa kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi katika vituo, changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni kwa kiwango kikubwa zimetokana na kutozingatia taratibu, kanuni na sheria zinazoongoza utambulisho wa mawakala wa vyama vya siasa,” alisema mwenyekiti huyo wakati akizungumzia uchaguzi huo.

“Wajibu wa kuwatambulisha mawakala upo kwa wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, si wajibu wa chama cha siasa kumtambulisha wakala wake kwa msimamizi wa kituo cha kupiga kura.”

Alisema matatizo hayo hujitokeza kwa sababu ya watu kutosoma vizuri sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza uchaguzi.

“Ndiyo maana leo tumesisitiza vyama vyote vya siasa vifuate taratibu zilizowekwa kwa ufasaha.”

Mwenyekiti huyo alisema maandalizi yanaendelea, huku akisisitiza kuwa baadhi ya vifaa vinavyohitajika katika hatua zote za uchaguzi vimeshaandaliwa, wasimamizi wa uchaguzi na wasaidizi katika ngazi za jimbo na kata wameshapewa mafunzo.

Hata hivyo alivikumbusha vyama vya siasa kuzingatia maadili ya uchaguzi ambayo yapo kwa mujibu wa sheria.

Hofu ya ADC, ACT

Awali katibu mkuu wa Chama cha ADC, Doyo Hassan alisema hawategemei mapya yatakayotokea katika uchaguzi huo, kwani purukushani na kupelekana polisi huenda vikatokea iwapo NEC haitafanya marekebisho yoyote.

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema hawana matumaini makubwa na wasimamizi kwa sababu kwa miaka mingi vyama vya siasa vimekuwa vikilalamikia uchaguzi kutokuwa huru na haki.

CUF wavuana uanachama

Wakati NEC ikijiandaa na uchaguzi huo, madiwani watatu wa CUF katika Jiji la Tanga wamevuliwa uanachama.

Waliovuliwa uanachama na kupoteza sifa ya kuwa madiwani ni Rashid Jumbe wa Kata ya Mwanzange pamoja na madiwani wa viti maalumu, Fatma Hamza na Halima Mbwana. Fatma pia alikuwa mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Tanga.

Akizungumzia hatua hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daud Mayeji alisema amepokea nakala za barua tatu zilizoandikwa na kusainiwa na kaimu katibu wa CUF, Magdalena Sakaya kwenda kwa madiwani hao kuwafahamisha juu ya suala hilo.

“Kwa hatua hiyo ni kwamba Halmashauri ya Jiji la Tanga ina nafasi tano za madiwani zilizo wazi, hawa waliovuliwa uanachama na waliojiondoa wiki iliyopita ambao ni Omari Mzee wa Makorora na Jumaa Ramadhani wa Kata ya Mabokweni,” alisema Mayeji.

Mkurugenzi huyo alisema jukumu lililobaki kwa sasa ni meya wa Jiji la Tanga kumjulisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi) kushughulikia mchakato wa kutangaza uchaguzi mdogo katika kata hizo na kuziba nafasi za madiwani wa viti maalumu.

Wakati Mayeji akitangaza hayo, Jumbe aliitisha mkutano wa wanahabari na kusema hatambui kuvuliwa uanachama kwa sababu Sakaya si mwanachama halali wa CUF.

“Kwanza bado sijapokea barua yoyote na hata ikiletwa kama aliyeandika na kutia saini ni Sakaya itakuwa ni batili, kwa sababu tulishamvua uanachama na hii inajulikana pia kwenye chama chetu hakuna wadhifa wa kaimu katibu mkuu, hivyo ameandika kwa kutekeleza kazi ya kukivuruga CUF,” alisema Jumbe.