http://www.swahilihub.com/image/view/-/4925944/medRes/1367368/-/9o3p15/-/msigwa.jpg

 

CCM, Mchungaji Msigwa waliamsha Iringa mjini

Mbunge wa jimbo la Iringa na mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa 

Na Berdina Majinge na Cledo Michael

Imepakiwa - Tuesday, January 8  2019 at  12:15

Kwa Muhtasari

Tunahitaji kufanya uchunguzi kwa nini jimbo lipo upinzani


 

mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Iringa. Vita ya kuwania Jimbo la Iringa Mjini imeanza mapema baada ya mwenyekiti mpya wa CCM mkoani humo, Dk Abel Nyamahanga kuahidi kulirejesha mikononi mwa chama hicho.

Hata hivyo, mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Peter Msigwa, amemjibu akisema hayumbishwi na kauli hiyo na kwamba CCM haiwezi kulichukua kwa kuwa Chadema ina wafuasi wengi.

Akizungumza juzi na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM baada ya kutangazwa mshindi, Dk Nyamahanga aliahidi kuwa atahakikisha jimbo hilo linarudi mikononi mwa CCM kwa njia yoyote akianza na kutatua changamoto za wananchi.

“Nashukuru kuchaguliwa kuwa mwenyekiti, ndoto yangu ni kuhakikisha navunja makundi ya baadhi ya wanachama na kuhakikisha tunaungana kuchukua jimbo kwa masilahi ya wananchi wanaokiamini chama kilichopo madarakani ambacho ni CCM,” alisema.

Mwenyekiti huyo alikuwa akirejea maagizo ya Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda ambaye ni mlezi wa CCM Mkoa wa Iringa aliyehoji kwa nini jimbo hilo liko chini ya chama cha upinzani na kuagiza katika uchaguzi wa 2020 lirudishwe CCM.

“Tunahitaji kufanya uchunguzi kwa nini jimbo lipo upinzani. 2020 ni muhimu likarudi CCM tu, nataka kujua je, ni wapigakura ndiyo tatizo au wanaCCM wenyewe tunashindwa kusimamisha mgombea tunayemtaka?” alihoji Pinda.

CCM wamuibua Msigwa

Akizungumza na Mwananchi jana, Msigwa ambaye alishinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na 2015, alisema haoni kama CCM ina ubavu wa kulichukua jimbo hilo. Msigwa ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, alisema katika mkoa huo wafuasi wa Chadema ni wengi zaidi na haoni kama chama chake kitapokwa jimbo katika Uchaguzi Mkuu ujao na kuwataka wanachama wake kuendelea kujenga imani kwa chama na viongozi mkoani humo.

“Tunajipanga vizuri kukabiliana na hali yoyote, hatutaki tupate mgombea mwepesi na tutawashinda kwa nguvu sana,” alisema.

CCM ilivyojipanga

Ili kupata ushindi, CCM imeainisha mipango yake kuwa ni pamoja na kuzunguka kata hadi kata kuzungumza na wananchi ili kutambua kero zao na kuzitolea ufumbuzi ikiwamo kujua idadi ya wapigakura wao.

“Uchaguzi huu (mkuu unaokuja) najipanga vizuri, nataka kuzungumza na wanaCCM kata kwa kata, mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji nijue changamoto zao (ili) kuhakikisha tunarekebisha makosa na kulikomboa jimbo hili,” alisema Pinda.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mgombea uenyekiti wa mkoa huo, Amani Mwamwindi amesema kwamba amekubali kushindwa.

Akizungumza jana, Mwamwindi alisema tofauti ya siasa na mpira ni kuwa, mpira una matokeo matatu ya kushinda, kushindwa na kutoka sare, lakini katika siasa ni kushinda na kushindwa, hivyo atamuunga mkono Dk Nyamahanga.