http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927298/medRes/2219199/-/so2n38z/-/bashiru.jpg

 

CCM yapunguza wapigakura za maoni

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally 

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  11:12

Kwa Muhtasari

Chama kitahakikisha mchujo unasimamiwa vizuri ili kuwapata wagombea safi

 

Bukoka. Zile harakati zilizokuwa zikishirikisha wanachama wengi wa CCM kila baada ya miaka mitano, sasa zitapungua baada ya chama hicho kuanzisha utaratibu mpya wa kura za maoni.

Badala ya wanachama wote kukutana katika mkutano mmoja na kupiga kura kuamua mgombea atakayepeperusha bendera ya CCM katika nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, udiwani au ubunge, sasa kutakuwa na wapigakura wachache.

Mabadiliko hayo yalidokezwa na katibu mkuu wa chama hicho tawala, Dk Bashiru Ally wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kagera mwishoni mwa wiki iliyopita.

Akizungumza na wanachama, Dk Bashiru alisema utaratibu wa zamani ulioshirikisha wanachama wote wa eneo la uchaguzi ulikuwa unahusisha gharama kubwa, kusababisha ununuzi wa kadi kwa ajili ya wapigakura na ulikuwa na upendeleo.

Hata hivyo, Dk Bashiru hakudokeza utaratibu utakaotumika kuwapata wapigakura za maoni, badala yake aliwataka wasiwe na hofu.

Dk Bashiru alisema chama hicho sasa kimeandaa utaratibu aliouelezea kuwa ni “mzuri” utakaowezesha kupata wagombea wenye sifa.

“Chama kitahakikisha mchujo unasimamiwa vizuri ili kuwapata wagombea safi,” alisema katibu huyo ambaye amekuwa akizunguka mikoani kufanya vikao vya ndani na wanachama.

Kwa utaratibu wa sasa, chama huandaa mkutano wa kura za maoni na wagombea hupelekwa kwa usafiri mmoja eneo hilo na kisha kujinadi na baadaye kupigiwa kura na wanachama waliojitokeza.

Wagombea wengi wa uongozi walikuwa wakijijengea nguvu ya kupata madaraka kwa kutumia mikutano hiyo ambayo anayeshinda anaweza kuzuiwa na Halmashauri Kuu ya CCM pekee.

Wenye nia walikuwa wakianza kujishirikisha katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa ajili ya kujenga uhalali kwa wanachama na baadaye kujijenga ndani ya chama, ikiwa ni pamoja na kuwakirimu na kuwawezesha kupata kadi na hivyo kuwa na nguvu katika eneo la uchaguzi.

Hata hivyo, katika uchaguzi wa wagombea uongozi wa uchaguzi mdogo uliofanyika sehemu mbalimbali mwaka jana, CCM haikutoa nafasi hiyo ya wanachama kupiga kura za maoni kupitisha wagombea, hasa waliotoka vyama vya upinzani. Badala yake, Kamati Kuu ya CCM ilikutana na kuwapa fursa wanachama waliojivua uanachama na kupoteza ubunge au udiwani, kugombea tena nafasi hizo, uamuzi ambao ulilalamikiwa na baadhi ya wanachama.