http://www.swahilihub.com/image/view/-/4801120/medRes/1990419/-/h8cgoaz/-/bashiru.jpg

 

Dk Bashiru aonya makada wanaoiponda CCM mitandaoni

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally  

Na Mwaandishi Wetu

Imepakiwa - Thursday, October 11  2018 at  12:07

Kwa Muhtasari

Atakayejadili masuala ya chama kwenye WhatsApp na akatapika nyongo na matusi, tutamshughulikia

 

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewaonya makada wa chama hicho wanaohamishia mijadala kwenye mitandao ya kijamii akisema watawajibishwa ili kukijenga chama hicho.

Aliyasema hayo wakati akichangia mjadala wa kumbukizi ya miaka 19 Tanzania bila Mwalimu Julius Nyerere uliofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam jana.

Huku akiutaja mtandao wa WhatsApp, Dk Bashiru alisema miongoni mwa mambo ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere ni dhana ya kujisahihisha, huku akiwaonya wanachama wa CCM wanaopeleka malalamiko mitandao ya jamii.

“Sisi kama chama tumeruhusu mijadala kwenye vikao halali badala ya kukaa kwenye mitandao ya WhatsApp. Atakayejadili masuala ya chama kwenye WhatsApp na akatapika nyongo na matusi, tutamshughulikia. Kwa sababu tunataka kujenga,” alisema Dk Bashiru.

Alisema hakuna uhuru wa kudharauliana, kusema uongo, kuchocheana na kudhalilishana kwa kisingizio cha kujadiliana.

“Hiyo haipo na mimi ndiyo msimamizi mkuu wa taratibu za chama, ujumbe umefika, lakini mijadala inayohusu kweli yenye dhamira njema watu wasiogope au kusingizia kwamba wanaogopa. Kwa nini ujifiche na jambo lako kama una nia njema. Kama umekosea utakosolewa kama mjadala,” alisisitiza.

“Lakini mijadala itatusahihisha, ndiyo maana Mwalimu aliweka dhana ya kujisahihisha. Katika nchi hii tumekosea mambo mengi. Tujadiliane tujisahihishe.”

Uzalendo wa Nyerere

Akizungumzia uzalendo, Dk Bashiru alisema uliofundishwa na Mwalimu Nyerere ni wa kitaifa unaounganisha makabila, tamaduni na dini. “Kwa hiyo tunapoanza kusifia uzalendo tuupe sifa. Uzalendo aliouhimiza Mwalimu ni wa kitaifa. Alitambua tunayo makabila mengi, tuna dini nyingi na tamaduni mbalimbali, lakini zote zikusanywe na utamaduni wa kitaifa tujenge Taifa,” alisema.

Katibu mkuu huyo alisema wananchi walipoacha kujadiliana masuala ukazuka uzalendo wa kibaguzi ukiwamo wa kikabila, kidini na wa kupenda vitu. “Tuwe wakweli, hii hali ipo na imekuwa wakati mwingine imekuwa na wakati wa kutisha. Mtu anatafuta uongozi anaanza kuwasiliana na kabila lake. Au mtu anaangalia kabila lake limepunjwa au limezingatiwa,” alisema

“Hivyo hivyo kwenye dini na siku hizi kuna ubaguzi hata wa kupenda vitu na anasa. Mtu anaiba lakini waliomchagua wanamwita jasiri, mjanja. Hiyo tukiizoea nayo inaweza ikawa uzalendo wa kusifu wezi.”

Awashangaa wanaompinga

Akichangia mjadala huo, Profesa wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Bernadetta Killian alisema anawashangaa watu wanaompinga Dk Bashiru kwa kuikosoa CCM wakati hata Mwalimu Nyerere aliwahi kuikosoa kwa utendaji wake.

Alisema kiongozi mzuri ni yule anayejikosoa hata mwenyewe kutokana na utendaji wake.

“Dk Bashiru alikikosoa chama chake alipokuwa mkoani Morogoro kwenye shughuli za kichama, lakini sasa watu waliposikia hivyo wakaja juu kweli nawashangaa kwa kweli,” alisema Profesa Killian.

Mkuu wa chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila alimtaka Dk Bashiru kuwahamasisha viongozi wa chama hicho kwenda chuoni hapo kusomea maadili na utawala bora. Alisema Mwalimu alianzisha viwanda ili kujenga Taifa imara linalojitegemea kiuchumi na viwanda vilivyoanzishwa vilikuwa ni vya nguo, kubangua korosho, kuchambua pamba na zana za kilimo.

Alisema viwanda hivyo vilikuwa na manufaa kwa Watanzania maskini na katika kilimo.

Kimiti akumbuka enzi zake

Waziri wa zamani, Paul Kimiti akizungumza katika kongamano hilo alisema wakati wa Mwalimu Nyerere walifundisha kuhusu uongozi bora. Alisema mwaka 1971 aliandika kitabu kilichokuwa kinahusu uongozi bora vijijini na alivigawa bure kwa wananchi na wengi wao wakiwa vijijini, lakini sasa viongozi wa kisiasa wanapiga kelele badala ya kutilia mkazo kilimo bora.

“Tulikuwa na vipindi Redio Tanzania, tulikuwa tunaelimisha wananchi kuhusu kilimo, lakini sasa viongozi wetu wa siasa hawatoi hata elimu hiyo kwa wananchi tena kama ilivyokuwa enzi zetu,” alisema Kimiti.

Kimiti aliyewahi kufundisha chuo hicho, mbali na kushika nyadhifa mbalimbali nchini alitoa wito wa kuwatumia wataalamu ili kutimiza falsafa ya Baba wa Taifa juu ya nchi kujitegemea na maendeleo ya viwanda nchini.

“Tanzania ina wataalamu wengi ambao wakitumika vilivyo, lazima lengo la falsafa hii ya Mwalimu itimie kwa sababu hata mimi kipindi kile alikuwa akinitumia kuwafundisha vijana kuhusu masuala ya siasa na kilimo na tulikuwa tukifikia lengo.”

Naye Buberwa Kaiza alisema hata msomi akiulizwa kuhusu dhana ya viwanda hawezi kutoa jibu la kueleweka na kwamba, wengi likizungumziwa suala hilo wanajua ni lazima kuwe na viwanda vikubwa.

Amfananisha JPM na Nyerere

Awali, akifungua mjadala huo, Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alimfananisha Rais John Magufuli na Mwalimu Julius Nyerere akisema amekuwa mstari wa mbele kupigania masilahi ya Taifa na kupambana na viongozi wanaokwenda kinyume na matarajio ya Watanzania.

“Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa mfano ambaye katika maisha yake aliweka mbele masilahi ya Taifa kuliko masilahi yake binafsi,” alisema Profesa Ndalichako.

Kongamano hilo lililokuwa na kaulimbiu ya Falsafa ya Mwalimu Nyerere Katika Kujitegemea na Maendeleo ya Viwanda Tanzania lilihudhuriwa na viongozi na wasomi kutoka taasisi mbalimbali nchini.