http://www.swahilihub.com/image/view/-/4928964/medRes/2149912/-/sql7m0/-/bashiru.jpg

 

Dk Bashiru awashtua madiwani, wabunge

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally 

Na Elias Msuya, Mwananchi

Imepakiwa - Thursday, January 10  2019 at  12:11

Kwa Muhtasari

Chama kitapata nafasi ya kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa kina kwa wagombea

 

emsuya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baadhi ya madiwani na wabunge wa CCM wameonyesha wasiwasi wa ongezeko la rushwa katika utaratibu mpya wa kura za maoni utakaopunguza idadi ya wajumbe wanaopiga kura ndani ya chama hicho.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara yake mkoani Kagera hivi karibuni, katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally alisema utaratibu wa zamani uliohusisha wanachama wote wa eneo la uchaguzi kushiriki katika kura za maoni ulikuwa na gharama kubwa, ulisababisha ununuzi wa kadi za chama kwa ajili ya wapigakura na uliambatana na upendeleo.

Licha ya kutoeleza utaratibu mpya utakavyokuwa, alisema chama hicho kimeandaa utaratibu mzuri utakaowezesha kupata wagombea wenye sifa na hautahusisha wanachama wote.

Hata hivyo, kauli yake haijapokelewa vizuri na wanachama na makada waliohojiwa na Mwananchi jana, na baadhi wanatofautiana.

“Utaratibu uliopo unahusisha wapigakura wengi, hivyo ilikuwa vigumu kwa mgombea kuwahonga kwa urahisi,” alisema diwani wa Mwandege wilayani Mkuranga, Adolf Kowero.

“Utakuta diwani unapigiwa kura na wajumbe 2,000, lakini sasa unapigiwa kura na wajumbe chini ya 200 labda 130. Mbunge alikuwa anachaguliwa na wanachama 15,000 lakini kwa sasa atachaguliwa na wanachama labda 2,000. Kama hao wajumbe hawatatoka na mgombea sahihi kwa kweli wataleta matatizo makubwa sana.

“Lazima chama kifanye ulinzi mkali sana wa rushwa kwani ni rahisi mgombea kuwanunua wajumbe wote.”

Alisema njia zinazotumiwa na wagombea kutoa rushwa ni wakati wajumbe wa mkutano wa kuchagua wagombea wanaposafiri kutoka matawini kwenda kwenye ofisi za chama za kata au za jimbo, akisema baadhi yao hutokea mbali kulingana na jiografia ya majimbo.

Mkoani Mwanza, diwani wa Hungumalwa wilayani Kwimba, Shija Marando alisema licha ya utaratibu mpya kusaidia kupunguza gharama, idadi ndogo ya wapigakura itaongeza mwanya wa rushwa.

“Kwa sababu mgombea atamudu kuwapa rushwa wajumbe. Zamani mgombea asingeweza kutoa rushwa, lakini sasa wenye fedha ndio watapata uongozi,” alisema Marando.

“Utakuta kila tawi lina wanachama 300 wanakuja kupiga kura, kata nzima ina wanachama labda 8,000 mgombea atawahongaje wanachama wote hao. Lakini wakiwa wachache itakuwa rahisi na wenye fedha ndio watapata uongozi,” alisema.

Kuhusu ununuzi holela wa kadi za CCM, Marando alisema umetokana na chama chenyewe kurahisisha utoaji wake tofauti na zamani.

“Zamani ili upate kadi ya chama ilikuwa lazima upate mafunzo kwanza, lakini siku hizi mgombea anakwenda kwa katibu wa chama wa kata anajieleza, anapewa kadi, anakwenda kuzigawa tu.”

Mbunge wa Nachingwea, Khamis Masala alisema licha ya kupunguza ushabiki kwenye chama, upunguzaji wa wapigakura utakiathiri.

“Chama kitapata nafasi ya kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa kina kwa wagombea kwa kuziba mianya ya rushwa toka kwa wagombea,” alisema.

“Uchache wa wapigakura utakwenda kutoa wagombea watakaokuwa na kazi kubwa ya kunadiwa kwa wananchi. Mtaji wa kwanza wa mgombea ulikuwa ni wanchama wenyewe.”

Alisema chama hicho kisipokuwa makini, rushwa itatamalaki kwa sababu ni rahisi kulipanga kundi dogo kibajeti.

“Chama kikipendekeza majina kwa ushabiki na kujuana kitapata changamoto kwenye chaguzi za nje na wapinzani,” alisema.

Felix Makene, aliyejitambulisha kama mwanachama wa CCM anayeishi jijini Dar es Salaam, alihoji aina ya wajumbe watakaopitishwa kuchagua wagombea akisema ni kuminya demokrasia.

“Kimsingi kura za maoni zinawapa wanachama demokrasia ya kuchagua wagombea, lakini wakisema wachache ndiyo wachague pengine wamepatikanaje? Je, kama hawamtaki huyo mgombea? Nadhani kura za maoni zihusishe wanachama wengi,” alisema Makene.

Lakini, diwani wa Kipili wilayani Nkasi, Wilbroad Chakukila ameusifu utaratibu huo wa kupunguza wapigakura akisema utazuia rushwa.

“Rushwa ipo tu, lakini sasa utaratibu utaibana zaidi kwani wataangalia umefanya nini kwa miaka mitano (ya uongozi),” alisema.

Mbunge wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita alisema licha ya kubadilishwa kwa utaratibu, CCM imebaki kuwa chama kinachopata wagombea kwa njia za kidemokrasia.

“Kila chama kina utaratibu wake, CCM kila mara inafanya chaguzi tofauti na vyama vya upinzani ambavyo wanakaa mezani na kuamua fulani ashike jimbo,” alisema Mhita.