http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759030/medRes/2109456/-/vukoua/-/seif.jpg

 

Jibu la Maalim Seif kwa Chadema laonyesha kulegeza msimamo

Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif  

Na Bakari Kiango

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  11:55

Kwa Muhtasari

Kiongozi huyo aonyesha kulegeza msimamo wake wa awali kuwa hawezi kuihama CUF

 

Dar es Salaam. Siku nne tangu Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chadema, Hashim Juma kumkaribisha Maalim Seif kujiunga na chama hicho akimuahidi kupitishwa kuwa mgombea urais wa Zanzibar, katibu mkuu huyo wa CUF amewajibu kwa maneno mafupi, “Muda ukifika nitazungumza.”

Baada ya kusema hayo alisema kwa sasa hayuko tayari kuzungumzia suala hilo.

“Siwezi kuzungumza na waandishi wa habari kwa sasa. lakini muda ukifika nitawaita na kuzungumza,” alisema Maalim Seif kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Zanzibar, Nassor Ahmad Mazrui.

Kauli hiyo ya Maalim Seif inashabihiana kidogo na iliyotolewa juzi na Mbunge wa Malindi kwa tiketi ya chama hicho, Ally Saleh ambaye alikaririwa na Mwananchi akisema wakati ukifika wataona cha kufanya alimradi wanabaki ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) unaoundwa na Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF yenyewe.

Saleh alisema hayo akijibu ombi la kiongozi huyo wa Chadema kwamba chama hicho kipo tayari pia kuwapa nafasi wabunge wote wa CUF endapo watajiunga nacho.

CUF ipo katika mgogoro ulioanza mwaka 2016, baada ya Profesa Lipumba kutangaza kurejea katika chama hicho, ikiwa ni mwaka mmoja alipojiondoa katika uenyekiti akisema anakuwa mwanachama wa kawaida kisha kutengeua uamuzi wake, licha ya mkutano mkuu kuikubali barua yake ya kujiuzulu.

Aidha, tamko hilo fupi la Maalim Seif linaonyesha dalili za kiongozi huyo kulegeza msimamo wake wa awali aliowahi kuutoa kwamba hawezi kuihama CUF.

Pia, hatua ya Maalim Seif kutakiwa Chadema imeonekana kumshtua Naibu Katibu Mkuu wa CUF-Bara, Magdalena Sakaya ambaye yupo upande wa Profesa Lipumba na jana alimshauri aachane na mpango huo, badala yake atulie ili alinde heshima yake.

Sakaya alisema ingawa suala la kuhama ni hiari ya mtu, itakuwa jambo la ajabu kama Maalim ataamua kuhamia Chadema kisha kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kama alivyoombwa.

“Akienda Chadema hawezi kushinda nafasi hiyo... akigombea upande wa Chadema itakuwa ni miujiza yeye kuibuka kidedea kwa sababu chama hiki hakina nguvu Zanzibar,” alisema Sakaya.

“Mimi kama mwanaye na yeye ni baba, nina mshauri atulie tu ili ajenge heshima yake kwa sababu aliwashawahi kuwa kiongozi mkubwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, (SMZ),” alisema.

Sakaya ambaye hivi sasa anakaimu ukatibu mkuu wa CUF baada ya Maalim kushindwa kuripoti makao makuu ya ofisi ya chama hicho, Buguruni Dar es Salaam kutokana na mgogoro uliopo, alisema endapo kiongozi huyo atakwenda Chadema atajiua kisiasa.

“Namuonea huruma ni bora atulie kuliko kumangamanga, lakini akienda kule (Chadema) ndipo kaburi lake la kisiasa lilipo. Itakuwa kichekesho cha mwaka, unaacha kuijenga nyumba yako unakwenda kuimarisha ya jirani,” alisema Sakaya.

Sakaya alidai kuwa wazee wa Chadema hawana nia ya dhati ya kumtaka Maalim, badala yake wanataka kujiimarisha wao na kwamba kiongozi huyo atakuwa kama ngazi ya wao kupandia ili mchakato huo ufanikiwe.