http://www.swahilihub.com/image/view/-/2959504/medRes/1140289/-/sm0bo6z/-/DNINVESTIGATES0110e%25282%2529.jpg

 

Mishahara: Moses Kuria aonya wabunge, madiwani wa Jubilee

Moses Kuria

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria (kati) akihutubu awali katika hoteli ya Boulevard, jijini Nairobi. Picha/GERALD ANDERSON 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Friday, December 8  2017 at  07:16

Kwa Mukhtasari

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amesema kuwa rais Uhuru Kenyatta hajafurahia kampeni za baadhi ya wabunge na madiwani za kuanza kujitafutia mishahara ya juu.

 

MBUNGE wa Gatundu Kusini, Moses Kuria amesema kuwa rais Uhuru Kenyatta hajafurahia kampeni za baadhi ya wabunge na madiwani za kuanza kujitafutia mishahara ya juu.

"Wale wote ambao wanajumuika ndani ya Jubilee wako na wajibu wa kutii viwango vya mishahara ambavyo vimetolewa na tume ya Sarah Serem ya kuthibiti viwango vya mishahara na marupurupu nchini,” amesema Kuria.

Kuria akiwa katika mahojiano na kituo cha redio amesema kuwa atazindua upya harakati za kuhakikisha wabunge wote na madiwani wa Jubilee wametii mwongozo huo.

“Juzi nilizindua harakati za kupunguzwa kwa mzigo wa kiuchumi kutoka kwa mwananchi wa kawaida na ambapo nilisukuma mishahara kutathiminiwa upya na tukaishia kukatwa mishahara hiyo. Ni lazima sote turidhike na viwango hivyo bila kulalamika,” amesema.

Amesema kuwa wote waliochaguliwa Agosti 8, 2017 waliingia afisini wakijua kwamba mishahara imepunguzwa na kwa sasa hawana lingine ila tu kuheshimu hizo hela ambazo zinalipwa kwa sasa.

Amesema kuwa wote ndani ya Jubilee ambao watanaswa wakisukuma mishahara yao iongezwe watakuwa wakianikwa hadharani na kuaibishwa machoni mwa umma na ikiwezekana, kufadhiliwe njama za kuwatimua mamlakani.

"Ni usaliti kwa manifesto ya Jubilee na pia kujituma kwa rais ambapo kwa pamoja tumeafikiana kuwa tutaheshimu viwango hivyo vya mishahara. Ukinaswa ndani ya Jubilee ukipigia debe nyongeza ya mishahara, basi hutakuwa wetu na tutakukana,” amesema.