http://www.swahilihub.com/image/view/-/4885752/medRes/2191635/-/nrbv1jz/-/lema.jpg

 

Lema anavyowapigania Mbowe na Matiko

Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema 

Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, December 7  2018 at  16:05

Kwa Muhtasari

Ni sawa tukaacha kila kitu na kuanza kupiga kelele kwa ajili ya haki za viongozi wetu

 

 

Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ameamua kulishikia bango suala la mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Lema anaonekana kuhisi hatari ya wawili hao kukaa muda mrefu gerezani kama ilivyomtokea zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya dhamana yake kukumbana na ubishi mkali wa kisheria uliofika Mahakama ya Rufani.

Mbowe na Matiko wako gerezani baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu kufuta dhamana yao kwa kile ilichoeleza kukiuka masharti. Jaribio lao la kupinga uamuzi huo lilikubaliwa na Mahakama Kuu, lakini upande wa mashtaka ukakata rufaa Mahakama ya Rufani, ambayo bado haijatolea uamuzi.

Lema sasa anatumia mitandao ya kijamii, hasa Twitter, ambayo ana wafuasi 75,700, na Instagram (122,000) kuendesha kampeni ya kupinga hali hiyo.

“Mitandao ya kijamii ni kama chakula hivyo unahitaji diet kwa ajili ya afya ya akili. Kuna wakati mambo muhimu yanayohusu haki hayapati kipaumbele isipokuwa ile mijadala ya kipuuzi. Kwa wanachadema wote diet yetu sasa iwe viongozi wetu walioko mahabusu,” ameandika Lema katika akaunti ya Twitter iliyovuta watu 367.

“Ni sawa tukaacha kila kitu na kuanza kuomboleza kwa kupiga kelele kwa ajili ya haki za viongozi wetu walioko mahabusu. Hatuwezi kuwa na kazi nyingine zaidi ya hii. Mahakama inapaswa kuona umuhimu wa hadhi yake (Mbowe) na sisi tuisaidie. Hakuna aliye salama kwa mwenendo wa aina hii katika nchi,” alisema katika twiti nyingine iliyopendwa na watu 536.

Lema pia amezungumzia mambo kadhaa ya kisiasa na kijamii, lakini ujumbe mkubwa umekuwa ni viongozi hao.