http://www.swahilihub.com/image/view/-/4759324/medRes/2109651/-/7xa5mlz/-/salama.jpg

 

Mgombea CUF ahoji sababu ya Meya wa Jiji kushindwa kusimamia ukisanyaji wa mapato

Mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ukonga (CUF), Salama Masoud akiwapungia mkono wananchi alipokuwa akihutubia 

Na Asna Kaniki

Imepakiwa - Friday, September 14  2018 at  14:27

Kwa Muhtasari

Alisema endapo atachaguliwa ataishawishi Serikali ijenge kiwanda cha nyama pamoja na cha matunda ili kuongeza ajira

 

Dar es Salaam. Mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ukonga (CUF), Salama Masoud amesema viongozi wa Chadema akiwamo Meya wa Jiji la Dar es Salaam wameshindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika jiji hilo.

Kwa mujibu wa Masoud, alitegemea jiji hilo ambalo limeshikiwa na Chadema lingekuwa na maendeleo lakini bado wananchi wake wapo katika umaskini.

“Unawezaje kuwa Meya wa Jiji halafu Rais anatangaza kuwa ukusanyaji wa mapato umepungua? Hii ni aibu,”alisisitiza.

Masoud ambaye alikuwa akizungumza katika mkutano wa kampeni za ubunge katika Uwanja wa Mbuyuni Chanika, alisema jiji hilo lingeweza kukusanya mapato mengi kupitia kwa uongozi wa upinzani lakini wameshindwa na badala yake wameliacha. “Unapewa fursa ya kuliongoza jiji lakini unashindwa kupigania vijana wapate vibali vya kuendesha pikipiki mjini ambapo vibali hivyo watavilipia lakini unamwachia Makonda anatupeleka anavyotaka,” aliongeza.

Alisema endapo atachaguliwa ataishawishi Serikali ijenge kiwanda cha nyama pamoja na cha matunda ili kuongeza ajira kwa vijana ambao wengi wao wanahangaika mitaani.