http://www.swahilihub.com/image/view/-/4657402/medRes/2040751/-/vd3mauz/-/kabidhi.jpg

 

Mwigulu akabidhi ofisi rasmi pamoja mambo matatu ya msingi

Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani akikabidhi taarifa pamoja na nyaraka kwa Waziri mpya wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani  

Na Bakari Kiango

Imepakiwa - Wednesday, July 11  2018 at  12:06

Kwa Muhtasari

Pia alimtakia mrithi wake kazi njema

 

Dar es Salaam: Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba amekabidhi rasmi ofisi, lakini akaacha ushauri wa mambo matatu kwa mrithi wake, Kangi Lugola.

Anataka utaratibu wa askari wa Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa mikataba ya miaka 12 uondolewe, kuunganisha kozi ili kuwasaidia askari kupanda vyeo na kutofautisha faini wanazotozwa madereva wa pikipiki, bajaji na magari.

Dk Nchemba aliachwa katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Julai Mosi na siku iliyofuata Rais John Magufuli alitoa sababu 13 zilizomfanya amuache.

Mbunge huyo wa Iramba Magharibi, ambaye alichukua fomu kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015, jana alijikita zaidi katika utendaji, masilahi ya askari wa jeshi hilo na baadhi kushindwa kwenda masomoni, akisema ndio maana walilenga kuunganisha kozi kama ilivyo kwa Jeshi la Magereza.

“Mfano akienda kusomea kozi ya ukoplo awe ameisomea pia inayofuata,” alisema Dk Mwigulu katika hafla hiyo jijini Dar es Salaam jana.

“Kwa sababu kinachofanyika ni kuunganisha mitalaa ili akimaliza asihitajike kusoma tena kwa ajili ya kupanda cheo. Kwa sababu cheo kina uhusiano wa moja kwa moja na mafao wakati atakapostaafu.”

Dk Nchemba ambaye pia aliwahi kuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, alimtaka Lugola kuendeleza mchakato wa kuandaa kanuni mpya zitakazotofautisha faini wanazotozwa waendesha bodaboda, pikipiki za magurudumu matatu na magari makubwa kama daladala.

“Hii ilikuwa moja ya ahadi yetu. Tuliona hawa vijana wa bodaboda wanapata tabu kunapokuwa na gharama zilezile za faini wakati wao wanabeba abiria mmoja,” alisema. Pia alimshauri Waziri Lugola kuondoa utaratibu wa polisi wa kufanya kazi kwa mkataba wa miaka 12, jambo alilosema linalalamikiwa na askari kwa kuwa linathiri mafao yao.

“Alisema kwa utaratibu huo, askari akistaafu anahesabika amefanya kazi ya kudumu baada ya kumaliza miaka hiyo tofauti na mwalimu,” alisema.

Pia alisema amemkabidhi Lugola bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2018/19 kwa kuwa ina mipango mingi.

Mbali na ushauri, Dk Nchemba pia alimtakia mrithi wake kazi njema, huku akikumbusha kuwa anahamia viti vya nyuma ambako atatekeleza moja ya majukumu ya mbunge ya kuisimamia Serikali.

“Nimeondoka uwaziri tu, lakini bado ni mbunge na wajibu wetu ni kuishauri Serikali. Basi mimi ni mjukuu wake nitaendelea kuisadia Serikali ya CCM,” alisema, ambaye anaongoza Jimbo la Iramba Magharibi kwa kipindi cha pili.

Kwa upande wake, Lugola alisema amefurahi kukabidhiwa kijiti hicho na kuahidi kuendeleza shughuli alizokuwa amezifanya mtangulizi wake.

“Katika mbio za kupokezana kijiti, ukipokea hutazami nyuma,” alisema Lugola, ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji na wakosoaji wakubwa bungeni.

“Unakipokea kijiti ukiwa unatazama mbele unakoenda na mwendo. Nimekipokea sasa ni kuendelea na safari ili kijiti kisonge mbele. “Nimemuomba (Dk Nchemba) aendelee kunipa ushirikiano kwa sababu amekaa katika wizara hii na kuna mambo anayoweza kunisaidia. Sina mengi sana ila ni kuendelea kufanya kazi kwa kujiamini baada ya kukabidhiwa ofisi.”

Akizungumza mara baada ya kuapisha viongozi mbalimbali aliowateua wakiwamo mawaziri, Rais Magufuli alieleza jinsi Waziri wa Mambo ya Ndani alivyoshindwa kushughulikia masuala 13.

Miongoni mwa mambo hayo kuwa ni sakata la mkataba baina ya Jeshi la Polisi na kampuni ya Lugumi Enterprises kwa ajili ya kuweka mashine za kielektroniki za kutambua alama za binadamu.

Hadi wakati ukaguzi unafanyika, kampuni hiyo ilikuwa haijakamilisha kuweka mashine hizo katika zaidi ya nusu ya vituo hivyo licha ya kulipwa takriban asilimia 90 ya malipo yote ya Sh37 bilioni.

Sakata hilo liliingia bungeni, lakini likapelekwa kwa kamati ndogo iliyoshauri Bunge liielekeze Serikali kulishughulikia.

Rais alisema Mwigulu hakushughulikia suala hilo tangu Bunge liiagize Serikali.

Sababu nyingine ni mkataba wa ununuzi wa magari 777 ya polisi, ambayo baadhi yalikwama bandarini hadi Rais alipotembelea na kutoa maagizo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani na ya Fedha kushughulikia.

Changamoto nyingine ni zile zinazolikabili Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ongezeko la ajali za barabarani bila ya kuwapo kwa hatua zozote za kuzidhibiti na usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, (NGO).

Baada ya kuenguliwa, Dk Nchemba alipotea hadharani kwa muda kabla ya kuibuka Kijiji cha Misigiri wilayani Iramba, Singida ambako alipokewa na wapigakura wake aliowaeleza kuwa anarudi kwenye klabu yake kuongeza bidii.