http://www.swahilihub.com/image/view/-/4335936/medRes/1904925/-/hh6xgi/-/naswada.jpg

 

Ndii: Sababu za Nasa kuvunja mabunge ya wananchi

Uhuru

Rais Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na kiongozi wa ODM, Raila Odinga Machi 9, 2018 katika Harambee House, Nairobi. Picha/JEFF ANGOTE 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Tuesday, March 13  2018 at  11:09

Kwa Muhtasari

Siku moja baada ya National Super Alliance (Nasa) kusimamisha shughuli za mabunge ya wananchi, muungano huo umesema hatua hiyo ni ya muda tu.

 

SIKU moja baada ya National Super Alliance (Nasa) kusimamisha shughuli za mabunge ya wananchi, muungano huo umesema hatua hiyo ni ya muda tu.

Mwanamikakati wa Nasa Dkt David Ndii anasema mabunge hayo yamefutiliwa mbali ili 'kuona' iwapo mkataba ulioafikiwa Ijumaa kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa Nasa Raila Odinga, utaheshimiwa.

Ameonya kuwa endapo juhudi za viongozi hao hazitazaa matunda, Nasa haitakuwa na budi ila kufufua upya mabunge hayo.

"Taifa hili limekuwa na historia ya usaliti katika maswala ya uongozi," ameeleza Dkt Ndii ambaye ni mshauri mkuu katika muungano wa Nasa mapema Jumanne kwenye mahojiano na runinga ya Citizen nchini Kenya.

Jumatatu, kamati ya utendakazi wa Nasa ikiongozwa na Dkt Ndii, ilitangaza kusitisha mabunge hayo ya mwananchi ili kuruhusu viongozi hao kuunganisha nchi hii iliyogawanyika kwa msingi wa kisiasa na ukabila baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017 na marudio ya urais Oktoba 26, 2017.

"Viongozi wetu wametuomba tuwape nafasi watekeleze wajibu wa kuunganisha taifa. Tunaona ni jambo la busara kufikiria kwa pamoja, hivyo basi tunasimamisha mabunge ya mwananchi kote nchini," alieleza kwenye ripoti ya pamoja ya kamati hiyo katika makao makuu ya Nasa jijini Nairobi.

Mnamo Ijumaa Rais Kenyatta na waziri mkuu wa zamani Odinga, waliafikiana kuweka kando tofauti zao za kisiasa ili kuunganisha taifa.

Kaunti 14 ambazo ni ngome kuu za Nasa zilikuwa zimepitisha mswada wa kuunda mabunge ya wananchi kwa msingi wa kutotambua uongozi wa Rais Kenyatta na Naibu Rais William Ruto (Jubilee).

Dkt Ndii hata hivyo, ameyataka mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kufuatilia kwa karibu mkataba huo, akisema yana ushawishi mkuu kuwakumbusha viongozi hao haki za wananchi.