Ngilu aomba kura za wenyeji awe gavana Kitui

Charity Ngilu

Gavana mteule wa kautni ya Kitui Bi Charity Ngilu. Picha/SALATON NJAU 

Na LAWRENCE ONGARO

Imepakiwa - Friday, February 17  2017 at  12:08

Kwa Mukhtasari

Kinara wa chama cha Narc Party, amewarai wakazi wa kaunti ya Kitui kumpa nafasi ili awanie kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 8, 2017.

 

KINARA wa chama cha Narc Party, amewarai wakazi wa kaunti ya Kitui kumpa nafasi ili awanie kiti cha ugavana katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 8, 2017.

Bi Charity Ngilu aliwarai wakazi wa Kitui wafanye unugwana kwa kumchagua kwani anaamini ana ujuzi wa muda mrefu katika uongozi.

"Mimi kama kiongozi wenu wa zamani nimetembea nanyi katika mawimbi mazito na kwa hivyo najiwasilisha mbele yenu ili mnipatie nafasi ya kuwa gavana wenu mwanamke," alisema Ngilu.

Alitoa ahadi kuwa iwapo atachaguliwa atahakikisha kuwa analeta utajiri kwa wakazi wa Kitui kwa kuwaletea rasilimani zote zinazohitajika.

Alisema kaunti ya Kitui imepitia shida nyingi hasa ukosefu wa maji, ajira, miundo msingi na uongozi mbaya.

"Mimi nataka tufanye kazi kwa pamoja ili kila mwananchi anayeishi Kitui apate haki yake bila kunyanyaswa na yeyote," alisema Ngilu.

Alisema kwa muda wa miaka minne wakazi wa Kitui hawajafurahia uongozi uliopo kwa vile wamekosa mambo mengi yanayolingana na hali yao ya maisha.

Kwa hivyo alisema njia mwafaka wa kubadilisha hayo yote ni kuona ya kwamba wakazi wa Kitui wabadilishe hali ya uongozi.

Aliyasema hayo mnamo Jumatano mjini Kitui alipozuru eneo hilo kwa minajili ya kukutana na wakazi wa huko na kuelewa shida zao.

Alisema iwapo atapata nafasi ya kuwa gavana  mwanamke atafanya juhudi kuona ya kwamba maji safi yanapatikana katika kila kijiji kwa kuhakikisha visima vingi vinachimbwa ili kuzuia shida ya maji.

"Jambo lingine muhimu ni kuona ya kwamba vijana wanapata ajira bila kurandaranda ovyo mitaaani huku pia mji wa Kitui ukipewa sura mpya kwa kuwaalika wawekezaji kutoka nje," alisema Bi Ngilu.

Alisema atafanya juhudi kuona ya kwamba fedha zinazotoka katika serikali kuu zinatumiwa vyema kwa unyunyizaji wa maji kwenye mashamba vijijini.

Mwelekeo tofauti

Hata hivyo siasa za Ukambani zinaonekana kuchukua mwelekeo tofauti kwa vile hivi majuzi kinara wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka, alimrai seneta wa Kitui Bw Joseph Musila aachane na azma yake ya kuwania ugavana wa Kitui huku akisema gavana huyo Bw Julius Malombe aachiwe nafasi akigombee kiti hicho.

Wakati huo pia  Bw Kalonzo alimtetea gavana wa Makueni Bw Kivutha Kibwana akisema pia aachiwe nafasi  akitetee kiti hicho.

Inadaiwa seneta wa Makueni Bw Mutula Kilonzo Junior anakimezea mate kiti cha ugavana cha Makueni.

Wachanganuzi wa kisiasa wanadai ya kwamba Bw Kalonzo ni sharti aweke nyumba yake ya Wiper sawa kabla ya waasi wengi kuchomoka kwani inasemekana viongozi wengi watawania viti na vyama vingine huku wakisema watajitafutia mahali pa kujituliza kisiasa.