http://www.swahilihub.com/image/view/-/3442414/medRes/1480685/-/2itkvcz/-/barua.jpg

 

Raila apewa darasa kuhusu siasa za amani

Njogu Barua

Mbunge wa Gichugu Bw Njogu Barua akihutubia wazazi katika shule ya upili ya mseto ya Kiamwathi awali. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, January 7  2017 at  09:41

Kwa Mukhtasari

Wabunge wawili wa Jubilee kutoka Kaunti ya Kirinyaga wamemtaka kinara wa Cord Bw Raila Odinga athibiti wandani wake dhidi ya kutumia lugha za matusi na dharau katika kampeni za kumpigia debe.

 

WABUNGE wawili wa Jubilee kutoka Kaunti ya Kirinyaga wamemtaka kinara wa Cord Bw Raila Odinga athibiti wandani wake dhidi ya kutumia lugha za matusi na dharau katika kampeni za kumpigia debe.

Wamemuonya Bw Odinga kuwa kuhusishwa na siasa za dharau na matusi ni sawa na kumtwika uhasama wa kijamii, suala ambalo haliwezi likamfaa
kwa lolote lile kubakia akiheshimika hata akiwa kinara wa upinzani.

Wawili hao ambao ni mbunge wa Gichugu Bw Njogu Barua na mwenzake wa Ndia Bw Stephen Ngari wakiongea mjini Sagana waliteta kuwa “hivi
majuzi kumekuwa na mtindo wa wafuasi wa Bw Odinga wa kutusi wote walio na msimamo tofauti kuhusu ufaafu wake kama rais wa Kenya.”

Bw Ngari alisema kuwa hata wingu la aibu halijatulia baada ya mbunge wa Mbita Bi Millie Odhiambo kumtukana rais Uhuru Kenyatta hadharani
akimtaja kama rais feki ambaye hawezi akatambulika na yeyote.

“Katika kutoa matamshi hayo, Bi Odhiambo anaweza kufikiria kuwa alikuwa anamjenga Bw Odinga lakini kinyume na hilo, ni kuwa alikuwa akimbomoa kisiasa. Huyu ni rais aliye na wafuasi wake waliompigia kura na wanaompenda kwa dhati. Ni Rais anayetambulika kikatiba kama umoja wa taifa. Kumtukana ni kuwatukana wote wanaompenda na wanaopenda ustaarabu wa usemi na vitendo,” akasema.

Alisema kuwa kuna hata walio ndani ya Cord ambao hawavutiwi na siasa za dharau na matusi na wanaweza wakauchukia mrengo wao wa kisiasa kwa
msingi huo.

Naye Bw Barua alisema kuwa hatua ya gavana wa Mombasa Bw Ali Hassan Joho kumkabili Rais kwa siasa za propaganda katika hafla ya umma mwishoni mwa juma ni sawa na kudharau bendera ya Kenya.

“Bw Joho angejituma kuthibiti hisia zake na ajiepushe na makabiliano yaliyomwangazia kama aliyemdharau rais. Waliotazama kanda ya video
hiyo akionekana kuchangamka ajabu kumuaibisha rais watakubaliana nami kuwa hilo halifai kamwe,” akasema.

Kupandisha joto

Walisema kuwa matukio hayo ya kupandisha joto la kisiasa kiholela bila kuzingatia maono pana ya taifa hili “ndiyo kiini kikuu cha miradi ya Cord kuonekana kuishia na makali kiasi kwamba hata wakiitisha maandamano wengi huyasusia.”

Akasema Bw Barua: “Sio wengi walio na ujasiri wa kutoa matamshi na dharau hadharani. Sio waangwana wengi wanaoweza kuonekana katika
maandamano ambayo mababu na nyanya wa kisiasa wanajilaza barabarani kana kwamba wamekambwa na makali ya uzazi…. Bw Odinga anafaa aelewe
kuwa anajiwekea vigezo vya uhusiano na jamii zingine iwapo atafanikiwa kuwahi kuwa rais au pia akiwa nje ya siasa.”