http://www.swahilihub.com/image/view/-/4927168/medRes/2154288/-/5opej8z/-/samia.jpg

 

Samia apewa jukumu la kuwasuluhisha RC, Katibu wa CCM

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan 

Na Suzy Butondo, Mwananchi

Imepakiwa - Wednesday, January 9  2019 at  10:02

Kwa Muhtasari

Viongozi hao wanatunishiana misuli ya kimadaraka

 

sbutondo@mwananchi.co.tz

Shinyanga. Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amekabidhiwa jukumu jingine na chama chake - CCM, kuwasuluhisha mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack na katibu wa chama hicho mkoani hapa, Haula Kachwamba.

Katika usuluhishi huo, Samia ataongoza jopo linalomhusisha pia Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudentia Kabaka.

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na wajumbe wa halmashauri ya chama hicho mkoa juzi.

Katika kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na viongozi na watendaji wa Serikali na chama hicho, alisema wamefikia uamuzi wa kuwapatanisha wawili hao baada ya kubaini kuwa migogoro na mivutano kati yao inakwamisha utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maendeleo.

“Kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya mkuu wa mkoa na katibu wa CCM mkoa. Baada ya jitihada za awali za kuutatua kushindikana, sasa litakuja jopo la Makamu wa Rais na Mwenyekiti wa UWT Taifa kulishughulikia,” alisema.

Alisema viongozi hao wa Serikali na CCM wanatunishiana misuli ya kimadaraka, jambo linalosababisha mifarakano ya ndani kwa ndani na hivyo kuathiri ufanisi wa kiutendaji na usimamizi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Tellack na Kachwamba walikana kuwapo kwa mgogoro kati yao huku kila mmoja akisema anatekeleza wajibu na majukumu yake.

“Sina tatizo lolote na mkuu wa mkoa. Ninachofanya ni kutimiza wajibu wa chama kushika hatamu kwa kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi,” alisema Kachwamba.

Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Tellack aliyesisitiza kuwa anasimamia utendaji serikalini huku mwenzake akifanya hivyo kwenye chama.

Awali, akitoa taarifa ya utendaji kwa katibu mkuu, Tellack alisema wanasimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.