http://www.swahilihub.com/image/view/-/4610326/medRes/2007410/-/jnfuclz/-/mashaka.jpg

 

Wakili CUF ataka amri ya mahakama kutenguliwa

Wakili wa bodi ya wadhamini ya chama cha wananchi (CUF), Mashaka Ngole akiongea na waandishi wa habari nje ya Mahakama  

Na James Magai

Imepakiwa - Wednesday, June 13  2018 at  14:46

Kwa Muhtasari

Waliamua kusikiliza upande mmoja bila sababu za msingi

 

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF), kambi inayoongozwa na Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba imepinga amri ya Mahakama kuizuia Benki ya NMB na benki nyingine zote nchini kutoa fedha za ruzuku ya Serikali.

Hayo yakijiri, upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad unasema wanaolalamika hawana hoja, hivyo waende mahakamani.

Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa amri kufunga akaunti za chama hicho za ruzuku ya Serikali, baada ya kutoa amri kuzizua benki zote nchini kutoa fedha za Serikali kwa ajili ya ruzuku kwa chama hicho.

Akizungumzia amri ya Mahakama, wakili Mashaka Ngole anayeiwakilisha CUF upande wa Profesa Lipumba alidai amri hiyo ni batili kwa kuwa maombi yaliwasilishwa mahakamani kinyume cha utaratibu na yalisikilizwa upande mmoja kinyume cha amri ya 37, Kanuni ya 4 na ya 5 za Mwenendo wa Mashauri ya Madai, ambazo zinazuia usikilizwaji na utolewaji wa uamuzi au amri ya upande mmoja.

“Kutoka mahakamani hadi Ofisi ya Msajili (ambaye ni mdaiwa wa kwanza katika maombi hayo) ni karibu sana, lakini waliamua kusikiliza na kutoa uamuzi wa upande mmoja bila sababu za msingi, kinyume na amri na kanuni za Mahakama za uendeshaji wa mashauri ya madai,” alisema wakili Ngole.

Alisema kwa hali hiyo, wameazimia kuchukua hatua za kuwasilisha malalamiko kwa Jaji Kiongozi ili amri hiyo itenguliwe, badala yake wadai wawasilishe maombi rasmi na pande zote ziitwe na kusikilizwa.

“Jana tulikwenda kuonana na Jaji Kiongozi, lakini hatukumkuta wala Jaji Mfawidhi kwa sababu wote wako Arusha. Kwa hiyo tunawasubiri warudi tuwasilishe malalamiko yetu,” alisema wakili Ngole.

Tofauti na Ngole, wakili Juma Nassoro anayeiwakilisha CUF upande wa Maalim Seif alisema wanaolalamika hawana hoja.

Alisema kilichofanywa na mahakama si kitu kipya, bali amri yake ilikuwa ni kukazia tu uamuzi wa Mei 29 dhidi ya Msajili wa Vyama. “Haya ni maelekezo tu ya Mahakama kwa benki kukazia uamuzi wake wa Mei 29. Lakini kama wanadhani kuwa wana hoja, basi waende mahakamani,” alisema Wakili Nassoro.

Mahakama katika uamuzi uliotolewa na Jaji Wilfred Dyansobera Juni 8, imetoa zuio kwa Benki ya NMB ambako kuna akaunti za chama hicho, na benki nyingine zote zilizoko nchini kutotoa fedha yoyote ya ruzuku ya Serikali kwa chama hicho.

Zuio hilo linatokana na maombi yaliyofunguliwa mahakamani na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kambi ya Maalim Seif dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Mei 29, Mahakama ilitoa amri kumzuia Msajili kutoa ruzuku ya Serikali hadi kesi zinazohusu mgogoro wa uongozi ndani ya chama hicho zilizoko mahakamani zitakapoamuliwa.

CUF imekuwa katika mgogoro wa kiuongozi tangu mwaka 2016 baada ya Profesa Lipumba kubadilisha uamuzi wa kujiuzulu wadhifa huo aliouchukua Agosti 2015, na badala yake kurejea katika wadhifa huo Septemba 2016.

Uamuzi wa Profesa Lipumba unaotambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ulikigawa chama hicho katika pande mbili na kusababisha kufunguliana kesi takriban 20 mahakamani.