Hatutaki wizi wa kura asilani, asema Raila

Raila Odinga

Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga akihutubu awali. Picha/KEVIN ODIT 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  17:22

Kwa Mukhtasari

Kinara wa chama cha ODM Bw Raila Odinga Jumatano ametangaza kuwa safari hii ya uchaguzi mkuu wa 2017 hatatoa mwanya wa kura zake kuibwa na washindani wake.

 

KINARA wa chama cha ODM Bw Raila Odinga Jumatano ametangaza kuwa safari hii ya uchaguzi mkuu wa 2017 hatatoa mwanya wa kura zake kuibwa
na washindani wake.

Amesema kuwa “tumejipanga na yeyote atakayethubutu kuiba ushindi wetu atakumbana na matukio ya kufedhehesha: Nasisitiza: Usithubutu.”

Aliahidi serikali ya Jubilee vita sawa na za siafu katika kumng’oa nyoka pangoni ambapo alisema “nyoka huyo akiumwa katika kila eneo la mwili, lazima atang’oka.”

Alizitaka ngome zake muhimu zigawane kwa kuuma nyoka huyo hadi aishie kutoka pangoni (mamlakani).

Akiongea katika mkutano wa umoja wa vinara wa upinzani katika ukumbi wa Bomas, Bw Odinga alisema kuwa uwaniaji wa urais wa upinzani umeandaa mikakati minne ya kuhakikisha hakuna chenga watapigwa katika matokeo ya uchaguzi huo mkuu wa Agosti 8, 2017.

Alitaja mikakati hiyo kuwa wote waliohitimu kuwa wapiga kura katika ngome za upinzani wamefanya hivyo katika zoezi linalozinduliwa wiki ijayo na tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Pili, aliwataka wafuasi wake wote wawe na umakinifu wa kufuatilia harakati zote za IEBC na serikali katika maandalizi ya siku ya kupiga kura.

“Ni lazima wafuasi wetu wote wawe macho na wazime jitihada zozote za kutuhujumu. Iwe ni katika usajili, uhifadhi wa rekodi za wapiga kura, usajili wa maafisa wa kusimamia kura hiyo vituoni na hata baadaye. Wapambane kuwa wahudu9miwe kwa njia ya haki na isiyo na mchezo wa hujuma,” akasema.

Alisema kuwa mada ya tatu katika mikakati hiyo ni kuhakikisha kuwa kura hizo zote zimepigwa wakati wa uchaguzi mkuu na zipigiwe upinzani.

Aliteta kuwa kukosa kujisajili na pia kukosa kujitokeza kuipiga kura hiyo ni sawa na kumwangusha atimize lengo lake kuu la kuishia kuwa Ikulu.

Mwishowe, Bw Odinga alisema kuwa suala nyeti litakuwa la kulinda kura hizo dhidi ya wezi katika hatua ya kuzihesabu na kuzitangaza rasmi.

“Hilo mniachie. Niko na uwezo wa kuhakikisha hazitachezewa. Timiza wajibu wako wa kujisajili na ku9ipiga kura hiyo yako. Nitailinda,” akasema.

Siasa za mchujo

Odinga kisha aliwataka wafuasi na wawaniaji wa nyadhifa kwa mrengo wa upinzani wadumishe umoja na wajitume kuhakikisha kuwa hawatasambaratika baada ya siasa za mchujo wa upinzani.

“Sote tutakuwa kwa serikali. Tutakupa la maana la kutekeleza ndani ya serikali tutakayounda. Tukikaa pamoja, tunaelewa wazi kuwa uwezo na nia tuko nayo kutimua Jubilee mamlakani. Ni utawala ambao hatuwezi tukauvumilia asilani,” akasema.

Kisha, aliwaongoza vinara Musalia Mudavadi (Amani National Congress), Kalonzo Musyoka wa Wiper na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya kujituma
kutimiza umoja wa upinzani ambapo Seneta wa Siaya aliwasomea maazimio kama kiapo cha umoja na wakiwa wameshikana mikono, wakakubali kuwa
watiifu.