http://www.swahilihub.com/image/view/-/3111106/medRes/727057/-/1r62op/-/DnEUTrip0104v.jpg

 

Karanja Kibicho: Sina habari kuhusu kiapo cha Odinga Desemba 12

Karanja Kibicho

Dkt Karanja Kibicho. Picha/MAKTABA 

Na MWANGI MUIRURI na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Friday, December 8  2017 at  06:43

Kwa Muhtasari

Katibu maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, amesema kuwa ana habari ya sherehe moja ya kitaifa ambayo itaandaliwa Desemba 12 hapa nchini - kwamba sherehe hiyo ni ile ya Jamuhuri na ambayo itaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

 

KATIBU maalum katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, amesema kuwa ana habari ya sherehe moja ya kitaifa ambayo itaandaliwa Desemba 12 hapa nchini - kwamba sherehe hiyo ni ile ya Jamuhuri na ambayo itaongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Desemba 12 ni siku ambayo ni ya kihistoria na imechapishwa rasmi katika gazeti la serikali kuwa ya kuadhimishwa kitaifa,” amesema Kibicho.

Amesema kuwa serikali kuu haitakuwa na hafla nyingine yoyote katika taifa nzima.

“Umeniuliza kama tunatambua kuwa kunaweza kuwa na sherehe mbili za kitaifa Desemba 12 ambapo kuna sherehe za Jamuhuri na sherehe za kuapisha kinara wa National Resistance Movement (NRM) kuwa na mamlaka zaidi kuliko aliyo nayo kwa sasa,” akasema.

Alijibu kuwa “hata wewe ningetaka uniambie unatambua siku hiyo kuwa imetengewa hafla gani na ambapo ni hafla zitakazoshirikishwa na serikali kuu katika Kaunti zote 47.”

Amesema kuwa rasmi serikali inatambua tu kushirikishwa kwa sherehe za Jamuhuri wala sio sherehe nyingine yoyote ya kitaifa.

“Kuapishwa kwa raia mmoja wa Kenya akituzwa mamlaka yoyote yale sio hafla ya kitaifa. Kiapo cha Odinga hata sikielewi kwa kuwa hata hajatutumia barua za mwaliko na hata wizara ya masuala ya kigeni haijatupa habari ya kuandaa ulinzi kwa wageni wa kimataifa katika hafla hiyo,” amesema.

Kibicho kwa simu na mtandao wa Swahilihub amesema kuwa ikiwa kuna kiapo cha Odinga kitakachoandaliwa Desemba 12, hadi sasa, basi amekiweka kuwa siri yake kuu na ni kama ni hafla ya kibinafsi ambayo "itatekelezwa nyumbani kwake wala sio kitaifa".

Usalama kuimarishwa

Msemaji wa serikali, Eric Kiraithe, naye kwa upande wake amehakikishia taifa kuwa usalama utaimarishwa vilivyo siku ya kuadhimisha sherehe ya Jamhuri Dei inayoadhimishwa Desemba 12 kila mwaka.

Kinara wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga mnamo Jumanne Novemba 28 alitangaza kuwa Desemba 12, 2017 ataapishwa kama rais huku mgombea mwenza Kalonzo Musyoka kama naibu rais.

Bw Kiraithe akihutubu jana Alhamisi kwenye kikao na waandishi wa habari Sheria House jijini Nairobi, alionya kuwa yeyote atakayezua rabsha Jumanne ijayo ambayo ni sikukuu ya Jamhuri atakabiliwa vikali na mkono wa sheria, ikikumbukwa kwamba Raila alisema ataapishwa.

"Wakenya wasitie shaka hata kidogo, watakaothubutu kuleta fujo maafisa wa usalama watakabiliana nao ipasavyo," akaonya msemaji huyo wa serikali.

Mikutano ya hadhara ya Nasa imekuwa ikishuhudiwa maandamano, pamoja na ghasia na hata watu kuripotiwa kufariki maafisa wa polisi wanapokabiliana na waandamanaji.

Wakati huohuo jana, Bw Raila akihutubu katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi alikokuwa ameenda kuwafariji baadhi ya familia zilizokuwa zimeenda kuchukua miili ya wapendwa wao waliofariki kwenye ghasia hizo, alikashifu serikali akisema imefumbia macho vifo vya wafuasi wa Nasa walioaga dunia ghasia zilipotokea baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na kura ya marudio ya urais ya Oktoba 26.

Kinara huyo aidha alinyooshea kidole cha lawama maafisa wa polisi, akiteta kuwa ndio kiini cha maafa hayo.

"Serikali imesalia kimya. Hakuna anayezungumzia kuhusu wafuasi wetu waliofariki kwa kupigwa na maafisa wa polisi. Tunataka izipe familia za waathiriwa fidia," alisema Raila.

Hata hivyo, idara ya polisi imekuwa ikijiondolewa lawama hizo ikisema waliouawa ni wahuni waliotekeleza wizi wa biashara za watu wakati wa maandamano.

Msemaji wa serikali Eric Kiraithe alishikilia kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha umelinda kila mwananchi. "Serikali ina wajibu wa kulinda kila Kenya pamoja na mali yake, haitakubali ghasia kuzuka. Tutaka amani iendelee kushamiri," akaeleza.

Aliongeza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha imeimarisha maisha ya wananchi, kupitia miradi ya maendeleo walioahidi Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto. Alisema kuimarisha uchumi, kuboresha elimu na afya, mazingira ndio nguzo kuu za serikali. "Hatutaki kuonesha taswira mbaya ya mwananchi kuwa akipewa Sh200 na mwanasiasa, lengo la serikali ni kila Mkenya ajisimamie," akasema.