http://www.swahilihub.com/image/view/-/2877330/medRes/1093249/-/pw6f26z/-/BDParliament1206.jpg

 

Wawakilishi EALA: Ripoti kamili kuwasilishwa bungeni leo jioni

Majengo ya Bunge

Majengo ya Bunge la Kitaifa jijini Nairobi. Picha/MAKTABA  SWAHILIHUB

Na CHARLES WASONGA

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  13:51

Kwa Mukhtasari

Ripoti kamili ya Kamati ya Pamoja ya Bunge inayoshughulikia uteuzi wa wawakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) itawasilishwa Alhamisi jioni katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

 

RIPOTI kamili ya Kamati ya Pamoja ya Bunge inayoshughulikia uteuzi wa wawakilishi wa Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) itawasilishwa Alhamisi jioni katika Bunge la Kitaifa na Seneti.

Haya yanajiri huku watu 27 walioorodheshwa kushindania nafasi hizo wakiendeleza kampeni za kuwarai wabunge na maseneta wawapigie kura.

Uchaguzi huo utafanyika Desemba 13.

Ripoti hiyo itawasilishwa katika mabunge hayo na wenyeviti wenza; Katoo Ole Metito (Kajiado Kusini, Bunge la Kitaifa) na Seneta Aaron Cheruiyot (Kericho, Seneti).

"Tumekuwa tukifanya vikao kushughulikia suala hili. Kamati yetu itawalisha ripoti leo (Alhamisi) jioni katika mabunge yote mawili. Nawaomba wenzetu kujadili ripoti hiyo kwa undani ili tuweze kukamilisha kibarua hiki cha kuteua wawakilishi wa Kenya katika Bunge la EALA," Bw Cheruiyot akasema.

Kulingana na sheria ya EALA wanachama wa bunge hilo huchaguliwa na mabunge ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kenya ndio taifa la kipekee miongoni mwa mataifa ya EAC ambayo haijachagua wawakilishi wake katika bunge hilo la wajumbe 54 lenye makao yake mjini Arusha, Tanzania.

Mataifa mengine kama Uganda, Tanzani, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini yamechagua wajumbe wao.

Bunge hilo haliwezi kufanya vikao vyake wala kuchagua Spika wake bila wawakilishi tisa kutoka Kenya.

Kikao cha kwanza cha EALA kilifaa kuandaliwa mnamo Juni mwaka huu lakini hatua ya Kenya kufeli kuteua wawakilishi wake ilisambaratisha mpango huo.

Hali ya vuta nikuvute kati ya mirengo ya Jubilee na Nasa kuhusu wasifu wa wateule ndio ilikwaza mchakato wa uchaguzi wa wajumbe hao kabla ya kukamilika kwa muhula wa bunge la 11.