http://www.swahilihub.com/image/view/-/3032804/medRes/1227943/-/vxx7wqz/-/DnRailaReligion1301%25287%2529.jpg

 

Raila: Mataifa ya kigeni yamevalia miwani vifo vya watu wasio na hatia

Raila akutana na viongozi wa kidini

Kinara wa muungano wa Cord Raila Odinga akutana na viongozi wa kidini ofisini mwake Capitol Hill, Nairobi Januari 13, 2016. Picha/JEFF ANGOTE 

Na SAMMY WAWERU

Imepakiwa - Thursday, December 7  2017 at  11:29

Kwa Muhtasari

Kinara wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga ameitaka Marekani na mataifa mengine ya kigeni kukoma kuingilia siasa za Kenya hasa "ikionekana wazi kuwa mlifumbia macho visa vya wafuasi wetu kuuawa bila hatia".

 

KINARA wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga ameitaka Marekani na mataifa mengine ya kigeni kukoma kuingilia siasa za Kenya hasa "ikionekana wazi kuwa mlifumbia macho visa vya wafuasi wetu kuuawa bila hatia".

Bw Donald Trump ndiye Rais wa Marekani, na mwanzoni mwa wiki hii serikali ya nchi hiyo ilituma mwakilishi wake kumshauri Bw Raila kusitisha azma yake ya kutaka kuapishwa Desemba 12, 2017 kama rais na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka kama naibu rais.

Marekani pia imeitaka serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto kulegeza msimamo wao wafanye mazungumzo ya upatanisho na Bw Raila ili kuondoa joto la kisiasa linaloendelea kushuhudiwa nchini.

Kulingana na kinara huyo ni kwamba Kenya ni nchi inayojivunia demokrasia yake, hivyo basi Marekani ikome kuingilia maswala ya ndani ya taifa hili.

"Marekani iache kusema tunakiuka katiba. Maswala ya Kenya ni ya Kenya na raia wake," akasema Bw Raila mapema Alhamisi akihutubu katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi ambapo alikuwa ameenda kufariji familia za walioaga dunia baada ya marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 wakichukua miili ya wapendwa wao.

Aidha Bw Raila amesema shida za Kenya zinafaa kutatuliwa na Wakenya ila si kwa kuingiliwa na nchi za ughaibuni. Amekiri kuwa Marekani ina ndoto nzuri za nchi hii ikitoa ushauri wake, japo amesema haina ruhusa ya kuingilia utawala wa taifa hili pamoja na maswala yake. "Masaibu ya Kenya yanatambuliwa na Wakenya pekee, hivyo basi ndio wanafaa kuyatatua. Hii ni nchi yenye demokrasia," akaeleza.

Kinara huyo amesisitiza kuwa yeye ndiye aliibuka mshindi katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 8, akikashifu tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) kuwa ilimpokonya ushindi wake kwa kumpendelea Rais Kenyatta na Naibu Rais Ruto wa Jubilee (JP).

"Agosti 8 sisi ndisi tuliibuka washindi, ushindi wetu ulikabidhiwa Jubilee," akasema.

Agosti 8 Bw Kenyatta na Ruto ndio walitawazwa washindi na IEBC kama rais na naibu rais mtawalia, japo Nasa ilipinga ushindi wao katika mahakama ya juu ambapo Septemba 1 iliagiza IEBC kuandaa uchaguzi mpya kwa siku 60.

Marudio ya uchaguzi wa urais yalifanyika mnamo Alhamisi Oktoba 26, Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto wakaibuka washindi licha ya kinara wa Nasa Bw Raila kutangaza kujiondoa kushiriki kwa msingi kuwa matakwa yake hayakuafikiwa. Mbw Kenyatta na Ruto waliapishwa mnamo Jumanne Novemba 28, kama rais na naibu rais. Raila amesema hatambui uchaguzi wa Oktoba 26 na viongozi hao, akiteta kuwa katiba na sheria za uchaguzi zilikiukwa.

"Nasa haitambui uchaguzi wa Oktoba 26 wala kuapishwa kwa Bw Kenyatta na Ruto kama rais na naibu rais," akasema Raila.

Siku ambayo viongozi hao waliapishwa, Raila alitangaza kwamba ataapishwa mnamo Desemba 12, 2017 kama rais naye mgombea mwenza Kalonzo Musyoka akiwa naibu rais. Hata hivyo, pendekezo la Rais limechukulia kwa hisia tofauti na kukashifiwa na wanasiasa wa Jubilee, huku Marekani ikimtaka akome kuendelea na mpango wake na badala yake afanye mazungumzo na Rais Kenyatta na Naibu wake Ruto.

Kinara wa muungano wa National Super Alliance (Nasa) Raila Odinga ameikashifu serikali akisema haitilii maanani vifo vya wananchi walioaga dunia baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8 na marudio ya urais ya Oktoba 26.

Ghasia zilizuka katika baadhi ya maeneo nchini baada ya uchaguzi huo na kusababisha maafa ya watu kadhaa.

Akihutubu mapema Alhamisi katika hifadhi ya maiti ya City jijini Nairobi ambapo familia za baadhi ya walioaga dunia kwenye ghasia za uchaguzi wa Oktoba 26 wameenda kuchukua miili ya wapendwa wao, Bw Raila ameteta kuwa serikali imefumbia macho maafa hayo.

Amesema kuwa hakuna yeyote kutoka serikalini ambaye amezungumza kuhusu vifo vya watu hao, na kwamba serikali ndio inafaa kuwa katika mstari wa mbele kuwafariji. "Hakuna yeyote ambaye ameongea kuhusu wafuasi wetu waliouawa. Tumesikitishwa sana na jinsi mambo yanaendelea," akasema.

Lawama

Kinara huyo aidha amenyooshea kidole cha lawama maafisa wa polisi akisema ndio walisababisha vifo hivyo.

Aidha Raila ameitaka serikali kuchukulia hatua maafisa waliohusishwa na mauaji hayo.

"Kwa chochote kile hakuna kitu kama mauaji yaliyotekelezwa na halaiki ya watu, serikali iombe msamaha wananchi kwa ujumla na familia za waliofiwa. Ichukulie hatua kali maafisa waliohusishwa na mauaji hayo," akaagiza.

Hata hivyo, idara ya polisi imekuwa ikijiondolea lawama hizo ikisema waliofariki walikuwa wahuni hususan waliotekeleza wizi wa biashara za watu wakati wa ghasia na maandamano ya Nasa.

Idara hiyo imeshikilia maafisa wake hawakuhusishwa na mauaji yoyote, ikijitetea mengine yalisababishwa na raia wenyewe kwa wenyewe haswaa waliokuwa wakilinda mali yao.

Joseph Boinnet ndiye Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi.

Nasa ilipinga uchaguzi wa Agosti 8 ambapo Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto waliibuka washindi, katika mahakama ya kilele. Mahakama hiyo Septemba 1 ilifuta ushindi wa Bw Kenyatta na kuagiza tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka (IEBC) kuandaa uchaguzi mwingine.

Aidha marudio ya uchaguzi wa urais yalifanywa Oktoba 26, na Rais Kenyatta na Naibu Rais Ruto wakaibuka washindi licha ya Bw Raila kujiondoa kushiriki kinyang'anyiro hicho kwa msingi kuwa matakwa yake hayakuafikiwa.

Nasa imeendelea kupinga uhalisia wa uchaguzi huo, ikikumbukwa kwamba Bw Kenyatta na Ruto waliapishwa mnamo Jumanne Novemba 28, kama rais na naibu rais mtawalia.

Raila alisema ataapishwa mnamo Desemba 12, 2017 kuwa rais na mgombea mwenza Kalonzo Musyoka awe naibu wa rais.

Jubilee imekuwa ikisuta Raila ikisema kuwa lengo lake ni kujumuishwa kwenye serikali ya nusu mkate.

Raila naye amekuwa akipuuza madai hayo akisema yeye hataki nusu mkate ila 'boflo nzima', akimaanisha awe rais.

Muda mchache baadaye, Mwanasheria Mkuu Githu Muigai amemuonya Raila dhidi ya kuapishwa ikizingatiwa "wewe hujatangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kama aliyeshinda kura".