Wabunge Mlima Kenya wataka SK Macharia asamehewe

SK Macharia

Mfanyabiashara SK Macharia atoa maoni yake kuhusu sheria za uchaguzi Nairobi, Januari 3, 2017. Picha/DENNIS ONSONGO  

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Saturday, January 7  2017 at  17:42

Kwa Mukhtasari

Mwenyekiti wa wabunge wa Mlima Kenya Bw Dennis Waweru amewataka wafuasi wa Jubilee Mlima Kenya wamsamehe bwanyenye Samuel
Kamau Macharia kwa kudai kuwa Mzee Mwai Kibaki hakushinda uchaguzi wa 2007.

 

MWENYEKITI wa wabunge wa Mlima Kenya Bw Dennis Waweru amewataka wafuasi wa Jubilee Mlima Kenya wamsamehe bwanyenye Samuel
Kamau Macharia kwa kudai kuwa Mzee Mwai Kibaki hakushinda uchaguzi wa 2007.

Bw Waweru amesema kuwa huo ndio msimamo wa wabunge wote wa Mlima Kenya na ambao umeafikianwa kupitia mashauriano ya kina.

Almaarufu kama SK Macharia na ambaye ni mumiliki wa kampuni ya Royal Media Services (RMS), amezua hisia kali Mlima Kenya ambapo kwa mitandao ya kijamii na kwa vituo vya redio vinavyotangaza kwa lugha asili eneo hilo amebandikwa nembo ya “Thu ya Ruriri (Adui wa Kijamii)”.

Tayari, mbunge wa Starehe Bw Maina Kamanda amemsuta Bw Macharia kwa matamshi makali ya kumwangazia kama anayevuna faida kutoka kwa jamii
ya Agikuyu kupitia uwekezaji, lakini kupeleka faida zake kuwafaa wapinzani na wakosoaji wa Agikuyu.

“Sio eti tumsamehe kwa kuwa anayopayuka kutuhusu yana zuito wowote, bali tumsamehe kwa kuwa hajielewi kisiasa na kubishana naye ni
kupoteza wakati muhimu wa kujipanga na kuendelea na Maisha yetu ya kuunda uthabiti wa kesho yetu,” akasema Bw Waweru kwa Swahilihub kupitia kwa simu.

Amewataka wenyeji wa Mlima Kenya waelewe kuwa Bw Macharia ako na uhuru wake wa kujiunga na mrengo wa kisiasa aupendao na kutekeleza mikakati ya kuufaa mrengo huo wake wa kisiasa.

Aliwakumbusha wenyeji kuwa Bw Macharia ako na umri wa miaka 75 kwa sasa na kwa kawaida uthabiti wake wa maamuzi huenda hauko ngangari na
unakumbwa na kuyumbayumba.

“Mzaliwa wa 1942 hapa Kenya hawezi kuchukuliwa kwa uzito haswa katika masuala ya kiteknolojia. Alisema kuwa alitumia ujuzi wa mitambo setilaiti kuafikia uamuzi kuwa Bw Kibaki hakushinda uchaguzi wa 2007. Mitambo hiyo kwa uhakika haiwezi kuwa chini ya utaalamu wa Bw Macharia
bali ilithibitiwa na wafuasi na washauri wake ambao ni wa upinzani,” akasema.

Masilahi ya SK Macharia

Alisema kuwa kwa sasa Bw Macharia amethibitishia watu wa Mlima Kenya kuwa uwekezaji wake unalenga kunufaisha masilahi yapi na kupitia safu
gani.

“Ni mwanasiasa aliye na uegemeo wake ndani ya nje ya mpangilio wa Mlima Kenya. Hilo ni lake na ako na haki ya kujiridhisha kisiasa. Nasi tuko na imani yetu kisiasa. Yeye ni mpinzani wetu tu bali sio adui wetu. Tutamsamehe lakini amefanya vyema kutuonyesha msimamo wake na tutachukua tahadhari,” akasema.