http://www.swahilihub.com/image/view/-/3514114/medRes/1532149/-/vnxgxuz/-/ba4a.jpg

 

Wandani Jubilee wapuuzilia mbali kongamano la NASA

National Super Alliance

Vigogo wa upinzani National Super Alliance (NASA) Musalia Mudavadi (kushoto), Kalonzo Musyoka, Raila Odinga, Moses Wetang'ula na Nick Salat wakiwa ukumbi wa Bomas Januari 11, 2017. Picha/JEFF ANGOTE 

Na MWANGI MUIRURI

Imepakiwa - Wednesday, January 11  2017 at  18:20

Kwa Mukhtasari

Wandani wa serikali ya Jubilee Jumatano wameupuzilia mbali mkutano wa upinzani katika ukumbi wa Bomas chini ya mwavuli wa National Super Alliance (Nasa) wakisema kuwa ‘haukunasa’ lolote la kushtua.

 

WANDANI wa serikali ya Jubilee Jumatano wameupuzilia mbali mkutano wa upinzani katika ukumbi wa Bomas chini ya mwavuli wa National Super
Alliance (Nasa) wakisema kuwa ‘haukunasa’ lolote la kushtua.

Wengine kama Bi Priscilah Nyokabi aliye mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Nyeri alipigia mtandao wa Swahilihub simu.

"Mnafuatilia hii outing (kuburahi) kwa hawa waliochanganyikiwa wa kunasa kisichonasika,” ameuliza Nyokabi.

Akasema: “Mimi niko hapa nikifuatilia hii Cord-sinema (kejeli kwa msingi wa michezo ya kuigiza ya Afro-Sinema) na ambapo sasa Seneta wa
Machakos Bw Johnson Muthama anatuambia twende kwa kitanda tukasakate ngoma tuzae viongozi.”

Alisema kuwa matamshi kama ya Muthama hutia ladha sarakasi za upinzani “kabla ya kujituma kwa upinzani tena baada ya uchaguzi wa 2017 ambapo
tutawashinda kabla ya nusu ya kura za Kaunti kuisha kutangazwa rasmi.”

Wakiongozwa na kinara wa wengi katika bunge la Seneti Prof Kithure Kindiki, walisema kuwa ulikuwa mkutano wa kawaida wa hadhara uliojaa
hotuba zisizo na mwelekeo wowote wa kutangaza kivumbi kuzinduliwa cha urais 2017.

“Mimi nilingoja nikachoka kuwaona wakituambia mpinzani wetu ni nani katika mrengo huo. Sisi tayari tumekuwa kwa miaka mitano sasa tukimwanika wazi mgombezi wetu ambaye ni Rais Uhuru Kenyatta. Mshindani wake hadi sasa miezi saba kabla ya uchaguzi ni nani? Hilo ndilo nilikuwa nangojea,” akasema Prof Kindiki.

Alisema kuwa “kile nilichoshida nikisikiza ni uongo, udaku na propaganda kutoka kwa wote waliokuwa wakitoa hotuba zao.”

Jukumu kuu

Alisema kuwa Wakenya waliokuwa na imani na mrengo huo “wamebakia wamechanganyikiwa kusikia wakiambiwa wao ndio wako na jukumu la
kuwaunganisha vinara hao.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wabunge wa Mlima Kenya Bw Dennis Waweru alisema kuwa “kwa sasa la maana ni kuwa hawakutangaza kuzindua
maandamano yao ya kawaida katika barabjara za hapa nchini.

Alisema kuwa kwa hilo wameonekana kuimarika kisiasa kwa kiwango cha wastani “kwa kuwa wangefanya kosa la kutangaza maandamano basi
hawangepata nafasi ya kuwaandaa wapiga kura wao kujisajili kuanzia wiki ijayo.”

Hata hivyo, alisema kuwa bado mrengo huo wa upinzani haujajitoa kwa utata wa kisiasa kwa kuwa “ilibainika wazi kuwa Bw Musalia Mudavadi
hayuko tayari kumwachia yeyote kugombea urais kwa muungano wa Nasa na pia Kinara wa ODM Bw Raila Odinga alisema kuwa kura zake hazitaibwa.”

Alisema kuwa hilo linakuambia bado ndani ya Nasa kuna mirengo mitatu hasidi “mmoja ukiwa ni wa Odinga, mwingine ukiwa wa Mudavadi na
wa tatu ukiwa wa Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula wa Ford Kenya ambao wameonekana kutemwa nje na ujio wa Mudavadi.”

Bw Dennis Waweru naye alisema kuwa “hata yule aliyejitokeza kuwakilisha upinzani kwa Naibu wa Rais Bw William Ruto na ambaye ndiye Katibu Mkuu wa Kanu Bw Nick Salat hakutambuliwa na alionekana kuwa bawabu katika jukwaa la vinara.”

Alisema kuwa hadaa za kisiasa kama hizo za Bw Salat ndizo zitaponza Nasa na “kwa uhakika huu ni muungano ambao hauendi popote.”

Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Moses Kuria aliwataka Musyoka na Wetang'ula 'wajichanue' mapema na “waondoke kutoka muungano ambao utaishia kuwatema nje. Ni bayana kuwa hata ikiwa kuna hesabu inafanywa ndani ya Nasa, walio na hisa ni Bw Odinga na Bw Mudavadi.”

Hasa alimuonya Bw Kalonzo kuwa “ni bayana uko kivyako ikizingatiwa kuwa hata ulizimwa kuongea kwa muda na wafuasi sugu wa Raila.”