http://www.swahilihub.com/image/view/-/5119448/medRes/2346398/-/11tanu7/-/mgodi+pic.jpg

 

Hatima mgodi wa Nyamongo mikononi mwa mawairi wawili

Na Peter Saramba na Beldina Nyakeke mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Friday, May 17  2019 at  10:45

 

Tarime. Mawaziri wawili, Dotto Biteko wa Madini na January Makamba wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) wamebaini udhaifu katika udhibiti wa maji yenye kemikali kutoka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara uliopo Nyamongo kwenda kwenye makazi ya watu, mito na vijito.

Viongozi hao jana walikagua mabwawa ya maji machafu yanayodaiwa kusababisha madhara kwa afya za binadamu na mazingira kutoka mgodini na mifereji iliyochimbwa kuyazunguka yasiingie kwenye makazi ya wananchi.

Akitoa maelezo kwa mawaziri hao, mtaalamu wa udongo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Dalmas Nyaoro alisema uchunguzi wa timu maalumu ya Serikali umebaini maji yenye kemikali yanatiririka nje ya mabwawa na kusambaa kwenye makazi ya watu.

Mtaalamu kutoka Tume ya Madini, Nchagwa Marwa aliunga mkono kauli ya Dk Nyaoro akisema, “Hata leo (jana) tumebaini walijaribu kuchimba mtaro pembeni kudhibiti maji yasivuke kwenda kwenye makazi ya watu, lakini walipogundua eneo hilo lina maji mengi, wakaamua kulifukia badala ya kufanya uchunguzi kubaini yanatoka wapi na iwapo yana madhara kwa afya na mazingira.”

Meneja wa afya, usalama na mazingira wa mgodi huo, Reuben Ngusaru alisema juhudi za kudhibiti maji hayo zinafanyika kila siku kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya Serikali.

“Pamoja na kuchimba mitaro kuzunguka mabwawa, mgodi pia hutumia utaalamu wa kupunguza maji hayo kwa njia ya mvuke, njia hii inapunguza ujazo na mkandamizo wa maji yanayoweza kupenya ardhini,” alisema Ngusaru.

Alisema njia hiyo inasaidia kupunguza zaidi ya galoni 4,000 za maji kila siku na hivyo kufanya bwawa lisielemewe.