Tahariri tarehe 3rd Machi, 2019 Hili la kondomu lisiturudishe tulikotoka

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile 

Imepakiwa - Monday, March 4  2019 at  09:48

 

 Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa ya upungufu wa mipira ya kujikinga na magonjwa ya zinaa, hasa Ukimwi na hali hiyo ilijitokeza zaidi mkoani Njombe, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi na ugonjwa huo hatari.

Taarifa hiyo ilisema mipira hiyo ya kondomu ambayo ilikuwa ikipatikana bure au kwa bei rahisi kutokana na programu mbalimbali za Serikali za kudhibiti Ukimwi. Sasa imeadimika na iliyo katika maduka binafsi inauzwa kwa bei kubwa ambayo si rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuimudu.

Hizi si taarifa nzuri kwa nchi ambayo ilishapiga hatua kubwa kudhibiti ugonjwa huo hatari unaoambukiza kwa njia ya damu, hasa wapenzi wanapofanya tendo la ndoa bila ya kutumia kinga hiyo.

Kwa miaka kadhaa, Serikali kwa kutumia programu zake mbalimbali, taasisi binafsi na nchi washirika, imekuwa ikiendesha kwa ufanisi vita dhidi ya Ukimwi kwa kuelimisha umma, kusambaza mipira hiyo bure au kwa bei nafuu kwa kutumia mifumo ambayo iliwezesha wananchi kuzipata kwa urahisi, kuhamasisha wananchi kupima ili kujua afya zao mapema na kuanza tiba.

Hakuna shaka kwamba jitihada hizo ndizo zilizochangia kupungua kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa kiwango kikubwa. Na hakuna shaka pia elimu ya kutumia mipira hii ni moja ya njia kuu za kupunguza maambukizi.

Katika maadhimisho ya ya Siku ya Ukimwi Duniani, ilielezwa kuwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi yamepungua kutoka asilimia 9.2 hadi asilimia 5.1, taarifa ambazo ni njema baada ya jitihada kubwa za miaka mingi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, maambukizi katika maeneo ya mijini ni asilimia 7.2 wakati katika maeneo ya vijijini ni asilimia 4.3, huku wanawake wakiongoza kwa maambukizi kwa asilimia 6.2 kulinganisha na asilimia 3.8 kwa upande wa wanaume.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Njombe, ambako taarifa za uadimu huo wa kondomu ziliibukia, ndiyo inaongoza kwa kuwa na maambukizi ya asilimia 11.4 ya VVU wakati Iringa ni asilimia 11.3.

Haya ni maendeleo mazuri na mafanikio makubwa baada ya jitihada kubwa za miaka mingi zilizoshirikisha wadau mbalimbali kiasi cha kuufanya umma uelimike na kujiepusha na kufanya ngono zembe, ambazo mara nyingi huchangia kuambukiza Ukimwi.

Hata hivyo, taarifa kwamba kinga hizo zimeadimika si nzuri na kusipofanyika jitihada za makusudi, tutarudi kule tulikotoka ambako watu wengi walipoteza maisha na kuacha familia zao zikiteseka na pengine zikijikuta zikishindwa kufanya shughuli nyingine za kujiendeleza na matokeo yake ni umaskini.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndungulile alithibitisha upungufu huo na kwamba ulisababishwa na mfumo uliokuwepo kwa wasambazaji. Alisema jukumu hilo lilikuwa likifanywa na wasambazaji binafsi lakini sasa limerudi ndani ya Wizara ya Afya.

Alisema awali Serikali ilikuwa ikitoa fedha kwa taasisi ambazo zilinunua mipira hiyo na kuisambaza sehemu mbalimbali, lakini sasa wizara ndiyo itabeba jukumu hilo la kusambaza na kuzigawa kwa taasisi zinazostahili.

Taarifa hiyo ya Dk Ndugulile pia ni habari njema, lakini ni vizuri basi Serikali ikahakikisha inashughulikia suala hilo kwa haraka ili mfumo mpya uwe na ufanisi kama uliokuwepo awali na hivyo upatikanaji wake uwe rahisi ili kuepusha wananchi kurudi katika tabia za awali za kupuuzia matumizi ya kinga hizo kutokana na kutoziona kirahisi na kwa bei nafuu.

Tulikotoka ni mbali na jitihada kubwa zimefanyika, kwa hiyo ni busara tukaepuka kurudi tulikotoka baada ya mafanikio haya makubwa ya kuelimisha watu kuhusu madhara ya kujamiiana bila ya kutumia kinga.