http://www.swahilihub.com/image/view/-/5122938/medRes/2348748/-/kw44b3/-/hoja+pic.jpg

 

Hoja zilizotikisa wiki ya saba ya Bunge la bajeti

Na Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz

Imepakiwa - Monday, May 20  2019 at  09:37

 

Dodoma. Wakati wabunge wakihitimisha kwa kupigia kura makaridio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, hoja saba zimetikisa katika wiki ya saba ya mkutano wa 15 wa Bunge.

Hoja hizo ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, kufutwa kwa mkataba wa kampuni ya ununuzi wa korosho ya Indo Power, Mbunge wa Ndanda (Chadema), Cecil Mwambe kumtuhumu Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya kwa Rushwa, kuchelewa kuanza kwa mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Nyingine ni mazingira mabaya ya biashara yaliyofanya biashara nyingi kufungwa, Hesabu za Ofisi ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kukaguliwa na Bunge na Mbunge wa Shinyanga (CCM) Stephen Masele kuamriwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kumsimamisha ujumbe wa Bunge la Afrika (PAP) kwa utovu wa nidhamu.

Hoja ya kusuasua kwa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambayo iliibuliwa na Mbunge wa Malindi (CUF) Ally Salehe ilichangiwa na wabunge wengi akiwamo Spika, Job Ndugai.

Wakati wabunge hao wakihoji, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe alisema majadiliano kati yao na Kampuni ya China Merchant Holding International Limited (CMHI) na State General Reserve Fund (SFRF) ya Omani, yanaweza kuendelea iwapo wataondoa masharti yasiyokuwa na maslahi na Taifa.

Mbunge wa Ulanga (CCM), Godluck Mlinga aliunga mkono Serikali kuangalia kwa makini kama masharti ya mkataba wa ujenzi yatakuwa na manufaa kwa Taifa.

“Lazima tuangalie pia masharti ambayo hayataliingiza Taifa katika matatizo na hayatamuumiza mwekezaji. Yasiwe masharti ya kutulalia moja kwa moja kwasababu hatuna uwezo hapana hata mimi ninaiunga mkono Serikali,” alisema.

Hoja nyingine ni ile ya kusitishwa kwa mkataba wa ununuzi wa Korosho kati ya Serikali na Kampuni ya Indo Power ya nchini Kenya iliyoingia katika makubaliano ya kununua korosho tani 100,000.

Wapinzani bungeni walitaka Serikali kuwawajibisha aliyekuwa waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamaganda Kabudi na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Florence Luoga kwa kulipotosha Taifa na kuingizia hasara kutokana na mkataba ambao haukufanyiwa upembuzi yakinifu.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Josephat Kakunda alisema viongozi hao walikuwa wageni waalikwa tu na wala hawakuhusika na makubaliano hayo.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Upendo Peneza alisema kama viongozi ni wale wale ambao hawafanyi uchunguzi kabla ya kuingia mikataba maana yake ni kwamba, nchi itaendelea kupata hasara licha ya kutungwa kwa sheria mpya ya kulinda raslimali nchini.

“Umakini lazima uwepo. Hili suala ni aibu kubwa sana kwa Serikali. Lazima wahusika wote waweze kujipima na kwa bahati mbaya sana, walituaminisha kuhusu uwezo wa hiyo kampuni jambo halikuwezekana,” alisema.

Aliitaka Serikali kuomba radhi pia wananchi wa kusini kwa hasara kubwa wamesababishiwa kwa kuchelewesha malipo yao ingawa korosho wameshapeleka.

Hoja ya Mradi wa Mchuchuma na Liganga kuchelewa kuanza ilionekana kuchangiwa na wabunge wengi waliotaka Serikali kuweka msimamo ni lini mradi huo utaanza.

Hata hivyo, Kakunda alisema mchakato wa kupitia upya mkataba huo unaendelea. Mazingira magumu ya kufanya biashaa nayo ilikuwa ilichangiwa na wabunge wengi ambao wamelisema biashara anyingi nchini zimefungwa na kwamba takwimu zinazotolewa na Serikali juu ya biashara zilizofungwa si halisi.

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Ashatu Kijaji alisema biashara zilizofungwa katika kipindi cha kuanzia Julai 2018 hadi Aprili mwaka huu ni 16,252 lakini zilizofunguliwa ni 147,818.

Naibu Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, Cecil Mwambe alisema mazingira ya kufanya biashar ahapa nchini ni magumu sana na kwamba ingawa Serikali inataja takwimu kubwa ya biashara zilizofunguliwa lakini wao wanachoangalia ni thamani ya biashara.

“Thamani ya biashara zilizofungwa tulinganishe na zilizofunguliwa.

Unaweza ukafunga duka kubwa la jumla lakini ukafungua grocery ya kuuza keki sida mtaani lakini hailingani na thamani ya biashara ulizofunga,”alisema.

Alisema hata wawekezaji wanaona mazingira magumu kwasababu hata sera za biashara nchini hazitabiriki kutokana na mabadiliko ya mara kwa mara ya sheria.

Mwisho