http://www.swahilihub.com/image/view/-/4961790/medRes/2239741/-/jieofy/-/ijuwe.jpg

 

Jaji Mkuu aeleza utakatishaji wa fedha haramu Zanzibar

Omar Othman Makungu

Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu. Picha/MAKTABA 

Na MUHAMMED KHAMIS, Mwananchi

Imepakiwa - Friday, February 1  2019 at  14:28

Kwa Muhtasari

Utakatishaji wa fedha haramu una athari hasi katika uchumi wa nchi yoyote ile na kwamba mapambano dhidi ya tatizo hilo hayataweza kufanikiwa iwapo jamii haitakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vyenye mamlaka husika.

 

UNGUJA

JAJI Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu amesema utakatishaji wa fedha haramu una athari kubwa katika uchumi wa nchi na kwamba mapambano dhidi ya tatizo hilo hayataweza kufanikiwa iwapo jamii haitakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo vyenye mamlaka husika.

Akizungumza Alhamisi mjini hapa, Jaji Makungu alisema utakatishaji wa fedha haramu una madhara makubwa ikiwamo kushusha uchumi hasa kwa mataifa yanayoendelea.

“Licha ya kurudisha nyuma harakati za kiuchumi, lakini pia tatizo hilo husababisha Taifa ambalo raia wake hujihusisha na shughuli hizo haramu kuchafuka kimataifa na kupoteza heshima yake,” alisema.

Jaji Makungu alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo majaji, mahakimu na makadhi wa Zanzibar juu ya namna ya kushughulikia masuala ya fedha haramu.

“Kwa kutambua ukubwa na athari za tatizo hilo, Serikali ya Zanzibar imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwamo kutunga sheria ya kukabiliana na vitendo hivyo viovu.”

“Jitihada za pamoja zinazochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na tatizo hilo zimeleta mafanikio makubwa,” alisema.

Alisema vitendo vya uhalifu na dawa za kulevya ambavyo ni miongoni mwa mambo yanayofanya utakatishaji wa fedha haramu vimekuwa vikidhibitiwa na kupungua kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Kamishna wa kitengo cha kudhibiti fedha haramu Tanzania, Onesmo Makombe alisema vitendo vya utakatishaji wa fedha haramu vinadhoofisha ukuaji wa uchumi wa nchi.

Alitoa wito kwa wananchi kuunga mkono mapambanao dhidi ya vitendo vya utakatishaji fedha haramu ili nchi iendelee kuaminika na kujenga imani mbele ya jamii ya kimataifa.

Sambamba na hayo alimhakikishia Jaji Mkuu wa Zanzibar kuwa kitengo cha kudhibiti fedha haramu Tanzania kitaendelea kutoa taaluma ndani ya pande zote mbili za Jumhuri ya Mungano wa Tanzania ili kuhakikisha tatizo hilo linapungua na hatimae kuondoka moja kwa moja.

 

Uelimishaji

Baadhi ya wananchi wakizungumza na gazeti la “Mwananchi” visiwani hapa walisema elimu kuhusu madhara ya utakatishwaji wa fedha haramu haikupaswa kumaliziwa kwa majaji na mahakimu badala yake ililazimika kushuka chini kwa wananchi wa kawaida.

Miongoni mwa waliosema hayo ni Khairat Abdulatif Mwanafunzi wa shahada ya kwanza ya usimamizi wa fedha kutoka chuo kikuu cha Zanzibar University ambaye alisema tatizo hilo linawakabili zaidi wananchi na baadhi ya viongozi au watu wenye fedha sasa anadhani taalumu hiyo ingeshushwa kwa watu wa kawaida hata kupitia makongamano maalumu ambayo yangeweza kuratibiwa.