Kasheshe la Fedha Bandia

Na Na Dennis Njalambaya

Imepakiwa - Tuesday, March 5  2019 at  16:25

 

Ilikuwa ni mwaka 1967 lilipotangazwa Azimio la Arusha ambalo liliwapiga kikumbo matajiri na mabepari waliokuwa na mali nyingi kupita kiasi. Azimio lilipotangazwa msambaratiko wa mabepari kuikimbia Serikali ya Nyerere ulikuwa mkubwa.

Wapo waliokimbilia Ulaya na Asia na wengine walivuka mpaka kwenda nchi jirani ya Kenya.

Kati ya matajiri wote hao, mmoja wao alikuwa Benson Papi, Mtanzania pekee aliyekuwa anakula sambamba na matajiri wa Kizungu waliokuwa sumu kali kwa Rais wa Awamu ya Kwanza wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere katika kuleta uwiano sawa kati ya matajiri na maskini.

Katika kukimbiza mali zao zisihodhiwe na Serikali, Benson Papi alihamia nchi jirani ya Kenya pamoja na familia yake na mali zake nyingi.

Huko Kenya hali ilimruhusu kuanza tena harakati zake. Harakaharaka alijenga hoteli kubwa tatu jijini Nairobi Mombasa na Kisumu. Hoteli zilimwongezea utajiri na umaarufu uliomfanya ajulikane Afrika na duniani kwa jumla kama tajiri katika nchi changa za Kiafrika zilizokuwa katika vuguvugu la kujitawala kutoka kutawaliwa na wageni.

Hali ya utajiri wa Benson  uliwavutia viongozi wengi wa Kiafrika wa wakati huo na kumshawishi mara kwa mara  awe anausaidia umoja huo wa Nchi Huru za Afrika (OAU) kutatua matatizo yaliyokuwa yanasababishwa na nchi kadhaa kutokuuchangia ipasavyo  umoja huo.

Katika hali yake ya kuwa na maendeleo makubwa  Benson bado alikuwa na ndoto ya kurudi Tanzania kulikokuwa na upinzani mkali wa Mwalimu Nyerere na mfumo wake wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, siasa iliyomlazimisha mtu kutokuwa na mali nyingi.

Hatimaye, Benson aliamua kukata shauri kuishiti Siasa ya Ujamaa na kuimarisha biashara zake zilizomwongezea utajiri mwingi. Katika hali hiyo, Benson akaingia katika maisha yake ya utajiri wa kupindukia na muda huo akaanza kuwindwa na majambazi hatari waliokuwa wanatamani fedha zake. Pesa iliyowavutia majambazi ilipiga hatua moja kwa kuibuka kwa makundi makubwa matatu hatari ya ujambazi yaliyomtingisha hata Rais wa Kenya  hayati Jomo Kenyatta hata akatoa ulinzi katika kikosi chake maalimu cha ulinzi kwa ajili ya kumlinda Benson ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa akijitolea  kuisaidia Serikali kama walivyokuwa matajiri wakubwa wa Ulaya.

Uamuzi huo wa Kenyatta ndiyo ilimwacha Benson akiwa huru na maisha yake  kwani makundi yote  ya ujambazi na washirika wake wote walitiwa mbaroni. Na hapo hapo Bension akaunda kikosi chake hatari cha ulinzi waliwamo mabodigadi wawili kutoka Cuba aliokuwa anaandamana nao muda wote.

Muda wote huo aliokuwa Kenya ulipita taratibu hadi mwaka 1987 uliporejea nchini katika kipindi cha uongozi wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi aliyekuja na mfumo wake wa kila siku wa ‘Ruksa’.

Uleule mrejesho wa kabla ya Azimio la Arusha, watu kujilimbikizia mali na mwisho Rais akawahamasisha wawekezaji  wazawa kuijenga Tanzania. Mfumo wa Ruksa ndio uliokuwa  chanzo kikubwa cha Benison kurudi Tanzania  kuanzisha miradi kama alivyokuwa anafanya Kenya. Hapa Tanzania alijenga hoteli za kitalii katika majiji ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam pamoja na ukumbi wa muziki wa aina yake hapa Tanzania.

Ikawa sasa ana miradi Kenya na Tanzania iliyomwingizia pesa zaidi. Katika miradi yake hiyo kwa jinsi siku zilivyokuwa zinakwenda, ndivyo mambo yalivyomchanganya na kuwatamanisha majambazi kuunda mbinu za jinsi ya kumuingilia Beason katika jumba lake la kifahari lililokuwa Masaki. Lilikuwa linalindwa saa 24.

Majambazi walianza kumfuatilia kila alikokwenda wakajipachika jina la ‘Ng’e Weusi’ ambao kabla walikuwa  wanawahenyesha matajiri mbalimbali wakitumia mbinu za kijambazi za nchi za  Ulaya.

Kati ya mbinu  zao, moja kubwa ilikuwa ni kuwateka watoto wa matajiri kisha kuwapigia simu wazazi wao na kutaka kitita kikubwa cha pesa ndipo  wawaachie huru watoto hao.

Kwa kiwango cha hali ya juu, mbinu zao zilikuwa zinafanikiwa na kuwaingizia pesa kutoka kwa idadi kubwa ya matajiri waliokuwa wanatoa kiasi kikubwa cha pesa kuwaokoa watoto wao.

Hali hiyo iliwapa kiburi ‘Ng’e Weusi’ kutamba kwa kiasi kikubwa na kuwahenyesha matajiri wa Dar es Salaam. Sasa wakapanga mbinu za kumwingilia Benson, tajiri aliyetosheleza kwa ulinzi mkali kuanzia ule wa nyumbani kwake hadi ule wake binafsi kwa kuwatumia Wacuba wawili.

Hali hiyo ya kufuatwafuatwa na ‘Ng’e Weusi’ alishaishtukia na kuanza kujilinda vyema na kundi hilo. Aliimarisha ulinzi kwa kuwachota walinzi wake wawili aliyopewa na aliyekuwa Rais wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.

Matamanio ya ‘Ng’e Weusi’ kundi linaloongoza na Michael Ngonge yalikuwa ni juu ya kumkamata Benson au mmoja wa watoto wake waliokuwa wanawawinda lakini ndiyo ikawa hivyo tena hawakuwahi kuwapata.

Benson alifikia hatua ya kutumia magari aliyoyapaka rangi nyeusi na bluu na kuyaandika  maandishi ya polisi ambayo yaliondoa kabisa ule morali wa ‘Ng’e  Weusi’ kuwakamata watoto wake  kwani walikuwa wanaamini kuwa magari anayotumia ni magari ya polisi.

Hivyo, Michael Ngonge aliwakusanya wafuasi wake na kuwakalisha chini  kubuni mbinu za jinsi ya kupata pesa  za Benson kiulaini tofauti na pale mwanzo walipomshtua naye akaanza kujilinda.   Siku ya Jumatano, Ngonge aliondoka katika jumba lake la kifahari lililoko Upanga na  kwenda Hoteli ya Sheraton.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                         Kwanza walitangulia vibaraka wake  wakiongozwa na Edson Wenda, Kasha Debe, Dioda Tumbo, Roshan Dule na Damas Didia. Kila mtu aliondoka na gari lake kwa muda wake na kwa njia tofauti. Wengine walipitia Barabara ya Magogoni, wengine katika barabara iliyopitia mbele ya Hospitali ya Aga Khan na baadaye kabisa kufuatia Michael Ngonge.

Michael alipofika alipaki gari lake aina ya BMW na kwenda ndani ya hoteli na kupanda hadi ghorofa ya nne  chumba na. 14. Chumba hiki alikilipia kwa wiki nzima. Alipoingia ndani aliwakuta wenzake  wakimsubiri. Naye alikaa katika kiti alichokuwa amekuja nacho. Alipokaa vizuri kitini alimwambia Edson Wanda kinara wa kundi lake kuufunga mlango  na dirisha kulikosababisha giza la wastani wa machweo ya jua.

Alipandisha spiringi za kiti chake hali iliyowafanya watu kuinua vichwa vyao  juu kumwangalia.

Akawasha taa iliyo chini ya egemeo ilikuwa ni taa yenye mwanga mkali iliyowalazimu watu wake kutokumwona vizuri. Alijiweka vizuri na kuanza maongezi. Lengo ni kujadili mbinu za kumwingilia Benson, tajiri anayenata hapa Tanzania ambaye kwa kiasi kikubwa ameonekana kuwa ni mtu bahili sana kutoa pesa. Hivyo, kikao hiki kilikuwa maalumu kwa kila mmoja kuchangia mawazo yake ya jinsi ya kumnasa Benson anayeatamia pesa kama kuku afanyavyo kwa mayai yake. “Je, nianze mimi au muanze nyie ?”

Itabidi uanze wewe mkuu! Edson alimpa fursa Ngonge aanze kutoa mawazo yake.

“OK, vizuri sana kwa kunipa nafasi hiyo. Mimi kwa mawazo yangu nina mbimu tatu za nguvu tutakazotarajia kuzifanya kwa ajili ya Benson. Mbinu ya kwanza ni kuimarisha maarifa ili tufanikiwe kumkamata Benson mwenyewe. Endapo tutamnasa itakuwa ndiyo huruma kutoka kwa mke wake kutoa pesa tutakazomtajia.

Mbinu ya pili ni kukamata mmoja wa watoto wake na mbinu ya tatu kumlazimisha kumpa ulinzi kama tunavyofanya  kwa matajiri wengine kama huyu  wa juzi Bwana Jonas Eric tulimpukutisha milioni kumi za haraka. Edson unasemaje?”

“Mimi naona nzuri zaidi ni kuwakamata watoto wake kuliko kumkamata mwenyewe kwa sababu watoto wake kutwa nzima wako shuleni. Hiyo ndiyo itakuwa fursa nzuri ya kuwakamata kwa kuwavizia wakati wa mapumziko.”

“Si unajua kuwa watoto wake wanatumia magari ya polisi tofauti na magari ya kawaida?”

“Nionavyo mimi Benson anatumia ujanja wa hali ya juu kutuhadaa. Jeshi la Polisi haliwezi kupoteza muda  kwa ajili ya kuwasafirisha watoto wa Benson wakati kuna mambo mengi ya maana yanayohitaji kufanywa kwa manufaa ya nchi. Mbinu aliyotumia Benson ni kuyafoji baadhi ya magari yake na kuyapaka rangi ya bluu na nyeupe pamoja na kuyaandika maandishi ya polisi ili tusiyaguse kwa kudhania kuwa  watoto wake wanasafirishwa na polisi.

“Yule anazuga tu.  Siku tujaribu kuvamia gari moja litakalobeba mmoja wa watoto wake. Hapo ndipo utaamini maneno yangu kuwa tunavugwa na yale magari mawili. Lakini njia nzuri si tungetumia ile ya kuwakamata watoto wake shuleni wakati wa mapumziko?”

“Hiyo kidogo itatia dosari. Kwanza watu  wengi watashuhudia kitendo kinachofanywa na hivyo kusababisha kufuatwa na walinzi watakaokuwa shuleni?

“Sasa njia gani tuitumie? Nia itakayotumika ni kuyavamia magari yake katika taa za kuongozea magari wakati magari yamesimama.”

“Halafu itakuwaje”

“Tutamlazimisha dereva aende kule tunakotaka sisi. Kwa maana hiyo, moja kwa moja tutampeleka  maskani huko tutamficha mtoto kwa siku kama tatu nne hivi. Kwa  lazima watatangaza kuwa mtoto wao amepotea.  Hiyo itakuwa fursa nzuri kuwasiliana na Benson atupatie pesa tunazotaka sisi kwa minajili  ya kumpata mtoto wake.

“Yaani najipongeza kwa kukiitisha kikao hiki ambacho kimefanikisha kupata mawazo  mazuri tofauti  na pale mwanzo ambapo mngekwenda kichwa kichwa katika mikono ya Benson ambaye hapana shaka muda huo mngekuwa mngekufa.”

Mimi naona mngetumia hii mbinu ya tatu ya kuvamia magari ambapo tutamteka mmoja wa watoto wake pamoja na dereva kwa jumla. Hapo umenena Edson na endapo mambo yatazidi kuwa mabaya tutalazimika kutumia silaha kutawanya kichwa cha dereva.”  

Tutakachofanya ni kuingia ndani  kimyakimya na kumtolea ‘changoma’ kitakachomlazimu kutii amri.”

“Na endapo kama mtakivaa kisiki mtachukua hatua gani? Kwa sababu haiwezekani Benson kutumia madereva wa kawaida. Ni lazima atawatumia walinzi wake.”

“Hao ndio viumbe tunaowataka. Pigo moja la nguvu ndilo litakalotumika  kumweka sawa  dereva atakayeleta matata. Sera zetu za kutumia vichwa vya watukutu ulitufundisha  mwenyewe na ndiyo tutakavyoitumia “

“Vyema mtatumia mbinu hiyo.”