Kasi ya dengue ituamshe kuchukua tahadhari

Imepakiwa - Tuesday, May 7  2019 at  11:27

 

Serikali imetangaza kugundulika kwa wagonjwa 1,222 waliougua homa ya dengue na vifo viwili zikiwa zimepita siku 24 tangu ilipotangaza kuwapo kwa ugonjwa huo nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema waliobainika ni kutoka mikoa ya Tanga, Singida na Dar es Salaam ambako kumeonekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wagonjwa.

Inaelezwa kuwa homa ya dengue inaenezwa na mbu aina ya Aedes Egypti ambaye huuma mchana na ingawa haambukizi malaria, lakini madhara yake kwa dengue ni hatari.

Japokuwa bado homa hiyo haijatazamwa kwa jicho stahili kwa maana ya kuwa na mikakati kabambe, lakini ni muhimu kufanya hivyo kwa ajili ya kuepusha hali mbaya zaidi inayoweza kujitokeza siku za usoni.

Jitihada za kuikabili homa hiyo zinapaswa kuongezeka katika ngazi mbalimbali kuanzia mwangalizi mkuu wa sekta ya afya kwa maana ya Serikali na hata mtu mmojammoja.

Serikali kupitia Dk Ndugulile, imesema tayari wameshaleta vitendanishi kwa ajili ya uchunguzi wa ugonjwa huo na kwamba wizara imeshaziagiza halmashauri kununua viuatilifu kwa ajili ya kupuliza katika maeneo yote yanayostahiki.

Kasi ya kuongezeka kwa homa hii imekuwa kubwa na kama itaendelea kuwa hivyo baada ya muda mfupi ambako kunaweza kushuhudiwa madhara makubwa zaidi.

Ni muhimu kupanua huduma ya upimaji na matibabu ya ugonjwa huo hususan katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za Serikali ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi hasa wenye kipato cha chini kupata huduma pale watakapoathiriwa na ugonjwa huo.

Hospitali za umma hasa zinazohudumia wananchi waliopo katika maeneo ya pembezoni zinapaswa kupewa uwezo zaidi wa kutoa matibabu ya dengue kwa kuwa gharama zake kuutibu katika hospitali au vituo binafsi vya afya ni kubwa, ambapo pia inaelezwa hazitoi huduma kwa wale wanaotumia bima ya afya kutibu homa hiyo.

Ni vyema juhudi kubwa zikachukuliwa hivi sasa wakati tatizo hilo halijafikia hatua mbaya na kusababisha madhara makubwa zaidi.

Elimu itolewe jinsi ya kujikinga dhidi ya dengue na endapo mtu atapata ugonjwa achukue hatua gani za haraka kabla hajapata madhara makubwa.

Wakati ni sasa kwa halmashauri kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alipozitaka kutenga fedha kwa ajili ya kununulia viuatilifu na kusambaza katika maeneo yote ili kuua mazalia ya mbu na wadudu wengine.

Kwa upande wa wananchi, wanapaswa kubeba wajibu kwa kuhakikisha wanapambana na dengue wakiondoa mazingira yanayochochea kuwapo kwa mbu kwenye makazi yao.

Pia, waripoti haraka vituo vya afya pale wanapojihisi kuwa na dalili za homa hiyo ambazo zinafanana na zile za malaria.

Tofauti na malaria, inawezekana kupambana na mbu wa dengue ikawa jambo rahisi kidogo kwa kuwa mmoja wa wataalamu kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), Dk Nicholaus Govela anasema mbu huyo huuma mchana wakati yule wa malaria huuma usiku.

Jamii iungane katika kupambana na homa ya dengue ili tusiendelee kupoteza nguvu kazi kwa wale watakaolazimika kukaa vitandani wakiugua au hata pengine kupoteza maisha kwa tatizo hilo.

Tunaamini iwapo kila upande utatimiza wajibu wake katika kukabiliana na homa hiyo, mafanikio ya kuudhibiti yatapatikana na kuondokana na hatari yake katika jamii, hivyo jukumu hilo lisiachwe kwa mtu au upande wowote. Ni vyema jamii ikajua kwamba, dengue ipo ‘kimyakimya’ lakini mapambano lazima yawe waziwazi.