http://www.swahilihub.com/image/view/-/5123494/medRes/2349303/-/xu1xajz/-/kichina+pic.png

 

Kichina kutahiniwa kidato cha nne

Na  Aurea Simtowe

Imepakiwa - Monday, May 20  2019 at  13:34

 

Dar es Salaam. Tangu kuanza kufundishwa kwa lugha ya Kichina nchini mwaka 2013, kwa mara ya kwanza Serikali imeingiza mtihani wa taifa kidato cha nne wa lugha hiyo kwa shule zinazofundisha somo hilo.

Kuanzishwa kwa mtihani wa somo hilo ni ishara ya kukua kwa lugha ya Kichina nchini, jambo ambalo pia linachochea kukua kwa ongezeko la wataalamu wa lugha hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kutoa mafunzo kwa walimu 81 kutoka China, Mkurugenzi msaidizi wa taasisi ya taaluma za Kichina ya Confucius Institute, Profesa Aldin Mutembei alisema hiyo ni hatua kubwa kuwahi kuchukuliwa na inadhihirisha umuhimu wa lugha hiyo.

Akimwakilisha makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Rose Upor amesema wanafunzi wanaosoma lugha ya Kichina wanapaswa kujua utajiri na faida ya tamaduni za Kichina duniani hasa katika kuchangia maendeleo.