http://www.swahilihub.com/image/view/-/3849650/medRes/1588633/-/5it8pk/-/pifa.jpg

 

Kikwete avalia njuga utawala bora, elimu, afya, vijana

Jakaya Kikwete

Rais wa Awamu ya Nne Tanzania, mstaafu Jakaya Kikwete. Picha/MAKTABA 

Na KALUNDE JAMAL

Imepakiwa - Tuesday, March 14  2017 at  17:08

Kwa Mukhtasari

Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete amezindua bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Jakaya Kikwete (JMKF) akisema lengo lake ni kusaidiana na Serikali na wananchi katika maeneo manne.

 

DAR ES SALAAM, Tanzania

RAIS wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete amezindua bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Jakaya Kikwete (JMKF) akisema lengo lake ni kusaidiana na Serikali na wananchi katika maeneo manne.

Akizungumza Jumatatu wakati wa uzinduzi wa bodi hiyo, Kikwete aliyataja maeneo hayo kuwa ni afya, elimu, vijana, maendeleo na utawala bora.

“Lengo la taasisi hii si kushindana na mtu bali tutashirikiana na taasisi nyingine, Serikali na wadau mbalimbali ndani ya nchi, barani Afrika na duniani kote tukihakikisha kuwa tunatimiza shabaha ya taasisi,” alisema Kikwete.

Kuhusu maendeleo alisema taasisi hiyo itasaidiana na wadau wengine kukabiliana na umaskini kwa kumsaidia mkulima mdogo, kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunafanya kazi kusaidia sekta ya afya na mtoto, kukabiliana na ugonjwa wa malaria kuboresha lishe ya wananchi kuboresha elimu katika kuwasaidia wajasiriamali kwa mafunzo na pia itasaidia katika utawala bora na utafutaji wa amani,” alisema.

Wajumbe wa bodi ya taasisi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sifue, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, Profesa wa Utabibu wa Hospitali ya Bugando, Mwanza, William Mahalu, Balozi Mwanaidi Majaar, Genevive Sangundi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Said S. Barkhessa, Abubakar Barkhessa.

Wengine ni Dato Sri Idris Jala wa Malaysia, Balozi wa zamani wa Marekani nchini Charles Stith na Dk Carlos Lapez ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).

Ufanikishaji

Akizungumzia uteuzi huo, Profesa Mukandala alisema atatumia uzoefu wake katika elimu kuhakikisha wanafanikisha malengo hayo manne muhimu.

“Nimekubali kwa moyo mkunjufu kuwa miongoni mwa watakaosaidia Watanzania na Waafrika kwa jumla katika nyanja mbalimbali,” alisema Mukandala.

Balozi Sefue alisema uteuzi huo ni heshima kubwa kwake na kuahidi kuyafanyia kazi mambo hayo manne.

“Nimefanya naye (KIkwete) kazi; nafahamu anapenda nini katika jamii inayozunguka ndani na nje ya nchi. Kutokana na kufahamu anataka nini nitashirikiana naye vizuri,” alisema Balozi Sefue.